Sh Bilioni 36 zatumika kwenye miradi ya maendeleo Manispaa ya Moshi

Miradi ya maendeleo yenye thamani ya jumla ya Sh Bilioni 36 imetekelezwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa kipindi cha miaka mitatu tangu Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mwajuma Nasombe, wakati wa kikao chake na Waandishi wa habari, alipokuwa akizungumzia miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika Manispaa hiyo.

Nasombe amesema Sh bilioni 36 zimetumika katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo miradi ya afya, elimu na uwezeshaji Wananchi  kiuchumi.

“Iko miradi mingi ya afya imetekelezwa, lakini pia kuna miradi ya elimu msingi na sekondari na miradi ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.”

Amesema kuwa Manispaa hiyo pia imejiimarisha kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani, hadi kufikia Juni 30 mwaka 2024 Manispaa hiyo imefanikiwa kukusanya mapato ya ndani zaidi ya bilioni 8.9 ambayo ni sawa na asilimia 101 ya malengo yaliyokuwa yamekusudiwa.

“Wakati naingia katika Manispaa ya Moshi, mwezi Desemba mwaka 2023, nilikuta ukusanyaji wa mapato ukiwa asilimia 32, kwa kipindi changu cha  miezi sita, tangu kuweko Manispaa ya Moshi, tumeweza kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka asilimia 32 hadi kufikia asilimia 69  na haya ni kati ya mafanikio ambayo tunaweza kujivunia,”amesema Nasombe.

Amefafanua kuwa mafanikio yote hayo ni uwepo wa ushirikiano anaoupata kutoka kwa Wataalamu wake ,Menejimenti na Baraza la Madiwani, Uongozi wa Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya, watu ambao wamekuwa wakimpa ushirikiano mkubwa.

Pia amesema Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, imetoa mikopo ya Sh bilioni 2.5 kwa makundi maalumu.

Katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia, halmashauri ya Manispaa ya Moshi, tumetoa mikopo takribani bilioni 2.5, vikundi 295 ni vya Wanawake, vikundi 100 ni Vijana na vikundi 22 ni vya Watu wenye mahitaji maalumu (walemavu).

Amesema, kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 Serikali kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) imetoa kiasi cha Sh bilioni 1.6 huku fedha nyingi zikienda kwa Wanawake.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, amesema kazi zilizofanyika katika kipindi cha miaka mitatu ya ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hssan, zitasaidia kuongeza kasi ya maendeleo kwenye Manispaa yetu ya Moshi.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.