TFS Moshi yaboresha miundombinu ya barabara, yajenga mahema Hifadhi ya Msitu wa Rau

 


Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, imeendelea na uboreshaji wa miundombinu ya barabara ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Rau, ili kuwezesha waongoza watalii kufanya kazi katika mazingira mazuri.

Mbali na maboresho hayo ya barabara pia wamenunua hema ambazo zinatumika kwa ajili ya kulala wageni katika hifadhi ya hiyo, hatua ambayo inatajwa kupunguza gharama za watu kwenda kukodi kwa makapuni binafsi yanayojishughulisha na masuala mazima ya utalii, jambo ambalo limesaidia kuchochea ongezeko la watalii kuja kutembelea katika hifadhi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake katika Kampeni ya Tukacharu msimu wa Pili, Ofisa Misitu daraja la Pili (TFS) Wilaya ya Moshi Zayana Mrisho Hashim, amesema malengo makubwa ya mpango kazi huo ni kuhamasisha utalii ikolojia pamoja na utunzaji wa mazingira na viumbe hai vilivyomo ndani ya hifadhi hiyo.

“Mtakumbuka kuwa katika mvua za masika mwaka huu, zilizonyesha zilisababisha miundombinu mingi ya barabara kuharibika, ziko juhudi mbalimbali ambazo tumeendelea kuzifanya, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara hatua ambayo inatupa ujasiri sisi TFS kuihamasiha jamii kushiriki katika utalii ikolojia kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali ndani ya hifadhi hiyo.”alisema Zayana.

Pamoja na juhudi kubwa zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan za kuutangaza utalii ndani na nje ya nchi idadi ya watalii imekuwa ikiongezeka katika msitu wa hifadhi ya Rau.

Alisema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Watalii waliotembelea hifadhi ya Msitu wa Rau walikuwa takribani 2,034 na mwaka 2023/2024 idadi hiyo iliongezeka na kufikia watalii takribani 6,651.

Aidha aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 wanatarajia kujenga nyumba za asili za kulala wageni (Cottages) pamoja na eneo la michezo kwa ajili ya watoto.

Kwa upande wake msimamizi wa msitu huo Kelvin Lubao, alisema msitu huo ni wa kipekee ambao ni mapafu ya mji wa Moshi, kwa kuwa unaboresha hali ya mandhari ya mji wa Moshi kwa kufyonza hewa ya kaboni, pamoja na kuhifadhi ardhi kutokana na miti iliyopo na utunzaji wa vyanzo vya maji ambayo yanatumika majumbani na mashambani.

Naye Ofisa Utalii TFS katika hifadhi ya Msitu wa Rau Jabir Nurdin, alisema mbali na wageni kunufaika na utalii ikolojia, ambao hufika kwa ajili ya kufanya matembezi ndani ya hifadhi hiyo, pia hushuhudia vivutio mbalimbali ikiwemo wanyama na chemchemi za maji.

“Kwa wale wanaokuja kufanya matembezi ya ndani ya msiti wa hifadhi wa Rau, wako wengine hujihusisha na uendeshaji wa baiskeli, ambapo hufanikiwa kuona baadhi ya vivutio vingi vinavyopatikana ndani ya msitu wa hifadhi Rau,”alisema. 

Akisoma makadirio ya bajeti kwa mwaka 2024/2025 Waziri wa Maliasili na Utalii Anjellah Kairuki, alisema Serikali itaongeza juhudi katika kuhamasisha utalii wa misitu unaotajwa kuwa wenye manufaa mengi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.