KIUSA, MOSHI
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro Zephania Sumaye, amezindua Mgahawa wa kisasa wa New Lumumba Restaurant, huku akitoa ushauri kwa Wananchi wa Wilayani humo, kutumia fursa za kiuwekezaji zinaotolewa na Chama cha Mapinduzi (CCM) ili kukuza vipato vyao na uchumi wa Wlaya kwa ujumla.
Kuzinduliwa kwa Mghawa huo, kunadhihirisha ukuaji wa uchumi wa Manispaa ya Moshi sanjari na utoaji wa fursa za ajira kwa Watanzania.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Moshi, ametoa ushauri huo Julai 19,2024, wakati akizindua Mgahawa wa Kisasa wa New Lumumba Restaurant, ulioko kwenye eneo la Ofisi ya CCM Wilaya ya Moshi Mjini, mkoani humo.
“CCM kwa nia njema kabisa yenye kuleta maendeleo ya nchi na watu wake imetoa fursa za uwekezaji kupitia chama hicho, ni vyema watu wakachangamkia fursa hizo ili waweze kukuza vipato vyao na hata kipato cha taifa kupitia kodi mbalimbali”, alisema DC Sumaye.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya, alimpongeza Mwekezaji aliyefungua Mgahawa huo Athuman Ally Mfutu, ambapo amesema Serikali itaendelea kushirikiana naye pamoja na wawekezaji wengine katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana Wilayani humo.
Akiongea katika hafla hiyo Naibu Mstahiki Meya Manispaa ya Moshi Stuwart Nathael, amesema uwekezaji huo utasaidia kukuza uchumi wa Manispaa ya Moshi kupitia njia mbalimbali kutokana na kukua kwa mzunguko wa fedha.
“Tatizo kubwa katika nchi yetu ni ukosefu wa ajira, inapotokea kijana anaamua kuwa Mwekezaji Serikali itamuunga mkono kwa kuwa atachangia kukua kwa uchumi”, amesema Nathael.
“Tunamshukuru sana Mkurugenzi wa New Lumumba Food Restaurant, kwa kuamua kuwekeza katika Mji wa Moshi, uwekezaji huu utakuza uchumi wa Wilaya yetu pamoja na kutoa fursa za ajira kwa vijana”, amesema.
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini Frida Kaaya, amesema chama hicho kinajivunia kupata mwekezaji huyo kwani atachangia ongezeko la mapato ya chama kupitia uwekezaji wake.
“Uwekezaji huu unatupa fursa ya kuendelea kubuni miradi mingine ya maendeleo ambayo itasaidia kukuza uchumi wa chama Wilaya”, amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Mjini Faraji Swai, amesema chama Wilayani humo, kitaendelea kushirikiana na Wawekezaji mbalimbali ili kuongeza fursa za uwekezaji Wilayani Moshi.
“Moja wapo ya yale yaliyomo ndani ya ilani ya CCM ni kwa serikali kutengeneza fursa za ajira; hili ndilo lililopelekea uongozi wa CCM wilaya kuja na wazo la kutafuta mwekezaji ambaye uwekezaji wake pia umebadilisha madhari ya ofisi kuwa nzuri”, amesema.
Awali akizungumza Mkurugenzi wa New Lumumba Food Restaurant Athuman Ally, amekishukuru Chama kwa kumpa ushirikiano katika uwekezaji alioufanya, ambapo amesema umetoa ajira kwa zaidi ya 15 wengi wao wakiwa ni vijana.