Babu; awataka wana-CCM kushirikiana na kukiimarisha chama

 

Kamisaa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, amesema mshikamano ndio nyenyo muhimu ya ushindi kwa chama hicho na kamwe kama wanachama wa CCM watashirikiana na viongozi wao walioko madarakani hawawezi kupata ushindi.

Akizungumza Julai 18,2024 na Viongozi wa CCM wa ngazi mbalimbali, kuanzia mashina, matawi, kata hadi wilaya, kwenye ufunguzi wa semina elekezi, iliyoandaliwa na CCM Wilaya ya Moshi MJini, mkutano ambao uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa CCM mkoani humo.

Amesema hakuna kitu kizuri katika shughuli za kisiasa kama kuwa na ushirikiano mzuri kwa viongozi na wanachama ili kuendelea kushika dola.

Amesema kutokuwa na ushirikiano huibua migogoro , jambo ambalo amesema halitarajii kulisikia na kuwataka viongozi na wanachama kuwa wamoja.

“Mshikamano ndani ya CCM, ndio nyenzo ya kwanza kwenye chama, kama Wanachama hawatashirikiana na viongozi wao ambao watakwenda kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, hawawezi kupata ushindi wa CCM,” amesema.

Aidha amempongeza Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini na Kamati yake ya Siasa, kwa maamuzi mazuri kwa kuwa wilaya ya kwanza kutoa semina hiyo kwa viongozi mbalimbali wakiwemo mabalozi.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini Faraji Swai, amesema semina hiyo, imelenga kuwajengea uwezo viongozi hao, ili watakapokwenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa yako mambo ambayo wanapaswa kuyafuata pasipo kuvunja kanuni za uchaguzi.

Awali akizungumza Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini Frida Kaaya, amesema katika kuelekea kwenye uchaguzi amewasihi wajumbe hao kuwa kitu kimoja ili kukiletea ushindi chama hicho.

Naye Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini Priscus Tarimo, amesema katika ahadi zake 10 ambazo, aliziahidi kwa wananchi, wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2020 nyingi zinaendelea kutekelezwa ikiwemo ukarabati wa uwanja wa Ndege Moshi, Ujenzi wa hospitali ya Wilaya na nyingine nyingi.

Amesema katika sekta ya elimu, Tarimo amesema zaidi ya madarasa 300 yamejengwa kwenye shule za msingi na sekondari, sanjari na ujenzi wa shule mpya za sekondari kwenye kata ambazi zilikuwa hazina sekondari.







 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.