Manispaa ya Moshi yapongezwa kwa ukusanyaji mapato 2023/2024


Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu akizungumza na Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Moshi mnamo Julai 3, 2024. (Picha na KISENA)

MOSHI, KILIMANJARO

Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imepongezwa kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato kutoka Sh Bilioni 6.9 mwaka 2022/2023, hadi kufikia  Sh Bilioni 8.9 mwaka 2023/2024.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, ametoa pongezi hizo Julai 3, 2024 alipokuwa akitoa salamu za Serikali katika Mkutano wa Baraza la Madiwani lililofanyika katika Ukumbi wa Manispaa hiyo  uliopo Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi.

Pamoja na pongezi hizo Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza zaidi katika ubunifu, bidii na nidhamu ya fedha za Serikali na katika uongezaji wa vyanzo vya mapato ili kuongeza wigo wa ukusanyaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iweze kutekelezwa kwa kasi zaidi jambo ambalo litawaletea maendeleo wananchi ambao ndiyo wenye miradi na fedha zao.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji Mkurugenzi mtendaji wa Manispaa hiyo Mwajuma Nasombe, amesema hadi kufikia Juni 30 mwaka 2024  Manispaa hiyo imefanikiwa kukusanya mapato ya ndani zaidi ya Sh Bilioni 8.9 ambayo ni sawa na asilimia 101 ya malengo yaliyokuwa yamekusudiwa.

Meya wa Halmashuri ya Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, ametaja ushirikiano miongoni mwa Madiwani Watendaji wa halmashauri na elimu kwa umma kuwa ni miongoni mwa siri ya mafanikio hayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Moshi Zephania Sumaye, ameupongeza uongozi wa halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa mafanikio hayo huku akiwataka kuongeza juhudi zaidi.

Naye Mwakilishi wa Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) Anord Kishimbo, ameutaka uongozi wa Manispaa ya Moshi, kuongeza bidii zaidi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.

Akizungumza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Mjini Faraji Swai,  amesema kwa muda mfupi ambao ameletwa mkurugenzi huyo, ameweza kupandisha mapato ya ndani kutoka asilimia 95 ya bajeti ya mwaka 2022/2023 mpaka kufikia asilimia 101 mwaka 2023/2024.

Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini Priscus Tarimo, amempongeza mkurugenzi na timu yake yote ya wataalamu, kwa hatua hiyo kubwa ya kuongeza ukusanyaji wa mapato, huku akisema kuwa endapo madiwani na watendaji wakaendelea kuwa na mshikamano wa pamoja Manispaa hiyo ina uwezo wa kuongeza ukusanyaji wa mapato mengi zaidi








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.