Kikosi cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, kimeanza tambo zake mapema za kunyakua ubingwa wa michuano ya ligi ya Zuberi Cup Tournament mchezo ambao unatarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni 19 mwaka huu katika Uwanja wa Mandela ulioko Kata ya Pasua Manispaa ya Moshi.
Hayo yamesemwa na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro Mkaguzi Jeremiah Mkomagi, wakati wa ufunguzi wa ligi ya Zuberi Cup Tournament 2024, ambapo ilishuhudiwa na uwepo wa mwasisi wa mashindano ya mpira ya mitaaa hapa nchini maarufu kama Ndondo Cup Shaffih Dauda.
Mkaguzi Mkomagi amesema kuwa, mwaka huu wamejipanga vyema kuhakikisha hawapotezi alama hata moja katika michuano hiyo, ili kuwasaidia kutwaa kikombe cha ubingwa huo.
“Mashindano ya mwaka huu, sisi Jeshi la Zimamoto na Uokoaji tunayo timu yetu ambayo inashiriki mashindano haya na siku ya Jumatano Juni 19, 2024 tunatarajia kushindana na timu ya Ng’ambo, tumejianda kuonyesha ushindani mkubwa na ikiwezekana kulichukua kombe hili mwaka huu,”amesema.
Aidha amewashukuru waandaji wa mashindano hayo, kwa jinsi ambavyo wameyaandaa, ili kuendelea kuibua vipaji vya vijana katika mji wa Moshi.
Michuano ya soka ya Zuberi Cup Tournament 2024 , yalianza kwa kishindo ambapo kulishuhudiwa mabingwa watetezi wa Pasua Big Stars wakipepetana na Wazalendo FC katika mchezo wa ufunguzi ambapo Pasua Big Stars iliibamiza Wazalendo FC goli 4-1.