Wadau wa Soka Kilimanjaro wamwagia sifa Rais Samia Suluhu Hassan



Wadau wa soka Mkoani Kilimanjaro, wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake kubwa anazozifanya katika kukuza sekta ya michezo hapa nchini, ambapo wamesema kuondoa kodi kwenye nyasi bandia zinazoagizwa toka nje ya nchi, jambo ambalo wamesema litachangia kukuza vipaji vya wanamichezo hususan wale walioko kwenye soka.

 

Aidha alisema kuwa kuondolewa kwa kodi kwenye nyasi bandia, utapelekea uingizwaji kwa wingi kwa nyasi hizo jambo ambalo alisema litawawezesha wachezaji haswa wanaokua kuonyesha vipaji vyao kutokana na uweko wa viwanja vingi vyenye viwango vya kuridhisha.  

 

Hayo yalisemwa Juni 16,2024 na Mratibu wa michuano ya Ndondo (Ndondo Cup) Shafii Dauda, wakati wa uzinduzi wa msimu wa nne wa michuano ya soka ya kombe la Zuberi Cup Tournament mwaka 2024 huku akimpongeza Rais Samia kwa namna ambavyo amejikita kwenye sekta ya michezo, ikiwemo hamasa kupitia zawadi mbalimbali ambazo amekuwa akizitioa katika kila timu iliyokuwa ikifanya vizuri katika Ligi Kuu iliyomalizika na hivyo kumechangia wachezaji wengi kujituma michezoni jambo ambalo litakuza michezo.

 

Alisema kuwa mbali na ahadi hiyo, Rais Samia amekuwa akidhamini michezo aina mbalimbali jambo ambalo pia limepelekea wana michezo kujitokeza wengi zaidi kushiriki kwenye aina ya michezo wanayoshiriki ukiwemo mchezo wa soka.

 

Aidha ametoa wito kwa wadau wa michezo kuunga mkono juhudi za Rais kwa kujitokeza kushiriki michezo kama wachezaji au  wafadhili ambapo alisema kwa kufanya hivyo sekta ya michezo itakuwa kwa kiwango kikubwa hata katika nyanja za kimataifa.

 

Akizungumzia michuano hiyo ya kombela Zuberi, Dauda alimpongeza mwasisi wa michuano hiyo ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo pamoja na kamati nzima kwa kuanzisha michuano hiyo ambapo amesema michuano hiyo ni hatua muhimu katika kukuza vipaji vya soka wilaya ya Moshi na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.

 

Akiongea wakati wa uzinduzi huo mwanzilishi wa mashindano hayo Diwani wa Kata ya Njoro Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, aliushukuru uongozi wa Chama cha soka Mkoa wa Kilimanjaro (KRFA) kwa ushirikiano ambao alisema imetoa na inaendelea kutoa kwa kamati ya mashindano hayo tangu yalipoanzishwa takribani miaka minne iliyopita.

 

Aidha Kidumo, alimpongeza Shafii Dauda ambaye ndiye aliekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo ambapo alielezea matumaini yake kuwa ushiriki wake utakuwa chachu ya kuendelea kukua kwa michuano hiyo kama ilivyokuwa ile ya Ndondo ambayo Dauda ni mratibu wake.

 

Nae Mratibu wa mashindano hayo Mwalimu Japhet Mpande alisema kuwa michuano hiyo inatarajiwa kushirikisha jumla ya timu 44 kutoka kata zote 21 za Manispaa ya Moshi na kwamba mshindi wa kwanza anatarajiwa kuondoka na jumla ya shilingi milioni 3, mshindi wa pili milioni 2 wakati mshindi wa tatu atapata zawadi ya shilingi milioni moja.

 

Awali Mwenyekiti wa soka Wilaya ya Moshi Abdallah Thabit, alitoa rai kwa wadau mbalimbali wa soka kuendelea kujitokeza kuandaa michuano ya aina mbalimbali ili kukuza soka wilayani humo na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.

 

Thabit ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa soka Mkoa wa Kilimanjaro Isack Munisi kwenye hafla hiyo alisema kuwa wandaaji wa mashindano ya kombe la Zuberi Cup Tournament 2024 wametimiza taratibu zote zinazohitajika na kwamba michuano hiyo ina Baraka zote za KRFA.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.