Vyama vya Ushirika Mbogamboga na Matunda vyataka ulinzi

Serikali  imeombwa kuvilinda Vyama vya Ushirika wa mazao ya mboga mboga na matunda mkoani Kilimanjaro, kwa kuwaondoa madalali ambao wamekuwa wakienda kwenye mashamba ya wakulima na kuwalangua kwa bei ya chini.

Wito huo umetolewa Juni 12,2024 na Viongozi wa Bodi za Vyama vya Ushirika wa mazao ya Bustani (Horticultural Amcos), ambao wanajishughulisha na  kilimo cha mbogamboga na matunda Mkoa wa Kilimanjaro, ambacho kinajumuisha mazao ya bustani kama vile nyanya, kabichi, spinachi, sukumawiki, Karoti, Ndizi bamia, tikiti maji.

Akizungumza Mwenyekiti wa Ushirika wa ndizi na matunda Wilaya ya Rombo, Amandus Assenga, ameyasema hayo wakati wa warsha ya mafunzo kwa viongozi wa Vyama vya Ushirika wa Mbogamboga na Matunda iliyoandaliwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Nchini TCDC.

Amesema wakulima bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya masoko ya mazao yao,  kwani  bado wameendelea kunyonywa kwa kulanguliwa mazao yao yakiwa shambani na madalali ambao huwapa bei ya chini na kuoimba serikali kuvilinda vyama hivyo ili mkulima aweze kunufaika na kilimo chake.

Amesema ili kuwanusuru wakulima na changamoto hiyo ameiomba Serikali kuondoa madalali, na wale wanaoleta makontena waweze kupita kwenye chama cha ushirika ili waweze kununua ndizi na maparachichi  kupitia ndani ya ushirika, ili  chama  kiweze kupata fedha ushirika na serikali kupata kodi yake lakini pia na mkulima aweze kunufaika.

Naye Fasila Ngalu kutoka chama cha ndizi Rombo, amesema uanzishwaji wa ushirika huo wa mbogamboga na matunda unakwenda kuwasaidia kupata sehemu ambayo wataweza kupeleka mazao ya wa ndizi na matunda.

Amesema  wanunuzi wanapoona ndizi zimekuwa nyingi hususha bei ya ndizi ambapo mkungu mmoja hulazimisha kununua kwa bei ya kwa Sh 2,000 hadi 3,000, lakini tukipata masoko ya ndani na nje, wakulima na wanaushirika kwa ujumla  wataweza kunufaika na mazao hayo.

Ngalu amesema mkulima ameendelea kunyonywa kwa kupewa bei ya chini na mnunuzi wa kati ambaye ni dalali, kuanzishwa kwa  huu unakwenda kumnufaisha mkulima  ambaye sasa ataleta mkungu wake wa ndizi kwenye ushirika na kuuza.

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Ushirika Uchira (Horticultural) Geofrey Mlay, amesema suala la masoko bado ni changamoto kubwa kwa wakulima wa mbogamboga na matunda na kwamba kwa kupitia warsha itakwenda kufungua fursa za kiuchumi kwa kupata masoko ya uhakika.

Mratibu wa mafunzo Kanda ya Kaskazini kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) Aurelia Mbwaga, ameeleza sifa za Wajumbe wa Bodi za Vyama vya Ushirika kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Ushirika akianisha baadhi ya sifa hizo ni pamoja na wajumbe wa bodi hzio kuzingatia kutokuwa na mgongano wa kimaslahi unaoweza kuathiri utekelezaji wa majukumu ya ushirika.

Aidha Mbwaga aliwataka viongozi hao kuhakikisha kwamba, wanalipa hisa zinazohitajika kwa mujibu wa masharti ya chama, ushiriki wa wajumbe katika vikao vilivyowekwa kwa mujibu wa masharti.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.