Kiwanda cha Sukari cha TPC kilichopo Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, kimeweka malengo ya kuzalisha zaidi ya tani 115,000 katika msimu mpya wa uzalishaji wa sukari kwa mwaka 2024/2025 ili kukidhi mahitaji ya walaji wa bidhaa hiyo wanaoishi mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
Ofisa mtendaji Mkuu na Utawala wa kiwanda hicho Jaffari Ally, akiongeza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya maombi maalumu, yaliyoandaliwa na wafanyakazi wa kiwanda hicho yaliyohusisha familia zao pamoja na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini.
Alisema katika msimu wa kilimo 2024/2025 TPC imeweka malengo ya kuzalisha tani 115,000 kutokana na uwepo wa tani 250,000 za miwa inayostahili kuvunwa katika msimu huo.
“TPC tumeanza uzalishaji wa sukari kuanzia Juni 3, 2024, ambapo tayari tumesha (TEST) ijaribu mitambo yetu yote na kuiona iko vizuri kwa ajili ya kuanza uzalishaji, tayari miwa tumeshaivunwa kwa kuanza uzalishaji na maji ya saa sita usiku kiwanda kitaanza uzalkishaji wa sukari,”alisema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Utawala wa kiwanda cha TPC Jaffary Ally.
Alisema msimu wa 2024/2025 wanayo miwa zaidi ya tani laki mbili na nusu elfu (250,000) ambayo ilikuwa inastahili kuvunwa msimu uliopita wa 2023/2024, ambapo sasa wanakwenda kuivunwa msimu wa 2024/2025 na hivyo kuongeza uzalishaji mkubwa wa sukari, kuliko kipindi chote cha nyuma.’
Alisema kutokana na uwepo wa ongezeko la uzalishaji wa sukari aliwataka wafanyabiashara na wasambazaji, kuacha tabia ya kuwalangua walaji wa bidhaa hiyo, kwani kutakuwa na sukari nyingi sana na ya kutosha kuliko ilivyowahi kuzalishwa miaka yote.
Aidha Ally, alisema msimu uliopita wa 2023/2024 kiwanda hicho kilishindwa kufikia malengo yake ya uzalishaji kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mvua za Eli-nino, zilizonyesha na kusababisha mashamba mengi ya miwa kuathiriwa, hali iliyopelekea kuzalisha tani 85,000 pekee za sukari.
Kuhusu changamoto za uingizwaji wa sukari kutoka nje ya nchi, Ally lisema kuingizwa kwa sukari hiyo kunaweza kuleta hatari ya kuua viwanda vya ndani.
Alisema sukari hiyo pia haijalipiwa ushuru na hivyo inaweza kuwa na tofauti katika bei ya sukari inayozalishwa na viwanda vya ndani na ile iliyoingizwa kutoka nje ya nchi.
“Tuko katika mazungumzo na Serikali ili kuweza kuhakikisha kwamba sukari ya ndani na yenyewe inapata soko sambamba na ile iliyoingizwa kutoka nje,”anasema Ally.
Wakizungumza kwenye maombi hayo baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho pamoja na viongozi wa dini wameeleza umuhimu wa wao kufanya maombi kabla ya kuanza msimu wa uzalishaji kiwandani hapo.
Msimu wa uzalishaji wa sukari kiwandani hapo utafikia tamati ifikapo mwezi Machi mwaka 2025 ili kupisha ukarabati wa mitambo inayozalisha sukari.