Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji Nchini (CGI) Dkt. Anna Makakala, amesema Jeshi hilo limefanikiwa kudhibiti wimbi la wahamiaji haramu waliokuwa wakiingia nchini bila kufuata utaratibu.
Dkt. Makakala ameyasema hayo Alhamisi ya Mei 30, 2024, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro wakati wa hafla ya kuwavisha nishani Watumishi wa Jeshi hilo 242 kwa mikoa minne ya Kanda ya Kaskazini waliyotunukiwa, awali na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Amesema wageni wengi waliokuwa wakitoka pembe ya Afrika kwa sasa wamepungua, baada ya kupata maelekezo kutoka kwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuweza kubadilisha kanuni za viza katika mataifa hayo.
Amesema Ethiopia na mataifa mengine yanayotoka pembe za Afrika kwa sasa wanaweza kuingia nchini kwa kufuata utaratibu rahisi, jambo ambalo litawezesha kuongeza mapato ya nchi na kupunguza idadi kubwa ya wageni ambao walikuwa wanaingia kiholela nchini na kulisababishia taifa hasara katika magereza.
Aidha amesema Jeshi hilo la Uhamiaji nchini imejiandaa kuwahudumia vyema Watalii wanaoingia nchini kwa ajili ya kutembelea hifadhi mbalimbali za taifa pamoja na usalama wao.
Amesema Jeshi la uhamiaji linaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya usalama katika kuhakikisha wageni watakaoingia nchini wanakuwa salama kipindi chote watakapokuwa hapa nchini.
Kuhusu hafla hiyo, Dkt Makakala amemshukuru Rais Dkt Samia kwa kutoa tuzo hizo ambazo amesema zitawapa ari watumishi wa idara hiyo kufanya kazi kwa bidii zaidi.
Wakiongea wakati wa hafla hiyo Mkaguzi wa Uhamiaji na Mkuu wa Wilaya ya Longido, mkoani Arusha Marco Ng’umbi na Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Uhamiaji ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Hai, mkaoni Kilimanjaro Sospeter Mabenga ambao walikuwa ni miongoni mwa watumishi wa umma waliovishwa nishani, wamesema nishani hizo ziwapa ari ya kutekeleza majukumu yao kwa nafasi ambayo waatakuwa wamepewa kuitumia serikali na umma kwa ujumla.
Aidha amempongeza Rais Samia kwa ujumla kwa kuboresha idara ya uhamiaji kwa kuongeza maofisa wapya na vifaa vya kisasa ambapo alisema maboresho hayo yameongeza ufanisi katika kazi zinazofanywa na jeshi hilo la uhamiaji hapa nchini.
Kwa upande wake Kamishna msaidizi wa Uhamiaji ambaye pia ni Afisa Uhamiaji Mkoa wa Tanga Kagimbo Hosea, amesema nishani hiyo imempa ari ya kutekeleza majukumu yake kwa nafasi ambayo amepewa kulitumikia Jeshi hilo
Wakati wa hafla hiyo jumla ya watumishi 242 wa Jeshi la uhamiaji kutoka Mikoa ya Arusha, Manyara, Tanga na Kilimanjaro, walivishwa nishani walizotunukiwa na Rais Dkt Samia, ambapo Kamishna Jenerali CGI Dkt Makakala aliwavalisha nishani hizo kwa niaba ya Rais Samia, hafla ilifanyika katika Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) kilichoko Moshi, mkaoni Kilimanjaro.