TCDC yatoa mafunzo kwa Bodi za Vyama vya ushirika wa mazao ya bustani

MOSHI, KILIMANJARO

Kujiunga  kwa sekta ya kilimo cha mboga mboga kwenye mfumo wa ushirika unatarajiwa kutoa mchango mkubwa kwa kukua kwa sekta hiyo hapa nchini na hvyo kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na seka ya Ushirika kwa ujumla.

Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushrika mkoani Kilimanjaro Jackline Senzige, ameyasema hayo Juni 10,2024 wakati akifungua mafunzo elekezi ya Wajumbe wa Bodi wa Vyama vya Ushirika vya mazao ya Bustani (Horticultural Amcos) kutoka wilaya ya Rombo, Hai, Moshi Manispaa na Moshi Vijijini  mafunzo yanayoendelea kwa siku tatu Mjini Moshi Mkoani humo.

Senzige amesema kuwa ushirika ni muhimu katika kukuza nguvu za kiuchumi za mtu mmoja mmoja na jamii yote kwa ujumla kupitia huduma za kiushirika zinazotolewa kupitia bidhaa za kiushirika aina mbali mbali.

Aidha ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha kwamba wanazingatia mafunzo hayo ili vyama vilivyoanzishwa viweze kuwa endelevu.

Senzige amesema kuwa mafunzo hayo yatawapitisha katika hatua mbalimbali zinazohusiana na uongozi ndani ya ushirika ikiwemo usimamizi wa fedha za ushirika huo.

Amesema kuwa mafunzo hayo pamoja na mambo mengine yatahusisha eneo la utunzaji wa mahesabu ya vyama vya ushirika ili vyama hivyo viweze kufanya vyema na hivyo kupelekea wanachama wake kupata mafanikio ikiwemo magwawio mazuri.

Aidha Mrajisi huyo Msaidizi Mkoa wa Kilimanjaro amesema kuwa kwa kuzingatia hayo na kuwa na ushirikaino mzuri kati ya viongozi na watendaji, sambamba na demokrasia wakati wa kufanya maamuzi ni wazi kuwa kutaimarisha vyama hivyo na ushirika wote kwa ujumla.

Awali akiongea kwenye mafunzo hayo, Mrajis Msaidizi Uhamasishaji na Uratibu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Nchini (TCDC) Ibrahim Kadudu, amesema kuwa washiriki wa mafunzo hayo watapata elimu mbalimbali inayohusiana na uongozi wa ushirika.

Amesema kuwa mafunzo hayo pia yanalenga kutoa mafunzo ambayo yatawawezesha wanaushirika wa mboga mboga kupata mafanikio ya kiuchumi kama yale wenzao waliyoyapaya kwenye sekta ya kahawa.

Amesema wakulima wa mboga mboga wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ile ya upatikanaji wa pembejeo, uhifadhi wa mazao, ukaushaji wa mazao, umwagiliaji wakati wa kilimo, mitaji, masoko ndani na nje; changamoto zote hizi zinaweza kupatiwa ufumbuzi kupitia mafunzo hayo.

Kwa upande wake Afisa Ushirika kutoka Tume ya Maendeleo ya Taifa (TCDC) Ndimolwo Laiser, amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga washiriki kutoka vyama vitano kutoka halmashauri nne zilizoko Mkoa wa Kilimanjaro, ambazo ni Hai, Rombo, halmashauri ya Wilaya ya Moshi (MDC) na Moshi Manispaa (MMC).










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.