Makamu wa Rais Dkt. Mpango ataka vijiji vya Same kupata Maji Safi na Salama

Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdori Mpango, ameiagiza Wizara ya Maji kuhakikisha vijiji vyote vinavyozunguka mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe, vinanufaika na maji safi na salama, yatokanayo na mradi huo.

Dkt. Mpango alitoa maagizo hayo Julai 14,2024 alipokagua mradi huo na kushuhudia wananchi wakianza kunufaika na maji yanayotokana na mradi huo ambao umefikia asilimia 95.

Amesema wananchi wanaozunguma mradi huo wakinufaika na mradi huo watatunza na kuvilinda vyanzo vya maji na miundo mbinu ya mradi huo kutokana na kuona faida yake.

Aidha Dkt. Mpango amewasihi wananchi wa Mwanga na Same, kuanza kutumia vyema maji hayo kwa kuhifadhi mazingira, ikiwemo kupanda miti katika maeneo yao yanayowazunguka.

“Wananchi mnaozunguka mradi huu wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe, hakikisheni mnakuwa walinzi wa mradi huo ili uweze kudumu na kuwanufaisha kwa kipindi kirefu, ninyi nyote mnatambua namna ambavyo mmeteseka kutafuta maji safi na salama kwa muda mrefu,”amesema Dkt. Mpango.

Vilevile Makamu wa Rais Dkt. Mpango amewataka viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro kuandaa malambo kwa ajili ya kunywesha mifugo ili kulinda mradi huo wa maji dhidi ya unyweshaji wa mifugo katika chanzo cha mradi huo.

Naye Waziri wa Maji Jumaa Aweso amewataka watendaji wa Sekta ya Maji kuhakikisha wana waunganisha wananchi wa Mwanga na Same huduma ya maji safi na salama kwa wakati na kutoa ankra sahihi kwa wananchi, wakati Wizara ikiendelea na utaratibu wa kufanikisha mita zamaji za malipo kabla.

Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kiarabu (BADEA), Mfuko wa Maendeleo wa Nchi Zinazozalisha Mafuta (OFID) na Kuwait Fund wanaendelea kutekeleza mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe ambao umelenga kusambaza maji katika Miji ya Same na Mwanga pamoja na vijiji 38 kwenye Wilaya za Same na Mwanga na vijiji vijiji vyote tisa vilivyopo katika eneo la chanzo cha maji vitapata maji.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.