Watu wasiojulikana wamedaiwa kuiba mita za maji kwenye nyumba za watu na kwenda kuziuza kama vyuma chakavu na hivyo kusababisha wakazi wa vitongoji vya Zilipendwa na Embakasi vilivyopo Mamlaka ya Mji mdogo wa Himo, kukosa huduma ya maji.
Akizungumza mmoja wa waathirika wa vitendo hivyo vya wizi wa mita Samweli Lyimo, amesema analazimika kwenda kuchota maji mtoni, kutokana na kukosa huduma hiyo, baada ya mita ya maji ya nyumba yake kuibiwa na watu ambao hadi sasa hawajatambulika.
Lyimo aliwaambia waandishi wa habari, kwamba wizi huo umetokea Mei 29 mwaka huu majira ya saa nane usiku, baada ya kusikia maji yakimwagika kwa kasi kubwa na alipotoka alikuwa mita ya maji imeibiwa.
Alisema baada ya kutokea wizi huo alienda kituo cha polisi Himo, sanjari na kuripoti kwa Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Moshi (MUWSA) kwa ajili ya kupatiwa mita mpya.
Mkurugenzi mtendaji wa (MUWSA) Mhandisi Kija Limbe, amethibitisha kutokea kwa wizi wa mita za maji 34 kwenye vitongoji vya Zilipendwa na Embakasi vilivyopo katika Mamlaka ya mji mdogo wa Himo.
Mhandisi Limbe alisema zipo hujuma ambazo zinaonekana kwa baadhi ya watu wasio waadilifu wamekuwa wakiziiba mita hizo na kwenda kuziuza kwa wafanyabiashara ambao hununua vyuma chakavu.
“Ni kweli kumetokea wizi wa mita za maji 34 ambazo zimeng’olewa kwenye makazi ya nyumba za watu katika vitongoji vya Zilipendwa na Embakasi vilivyopo Mamlaka ya Mji mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro na kusababisha wakazi hao kukosa huduma ya maji.”alisema.
Alisema tayari Mamlaka imeanza kuchukua hatua kwa kulishirikisha jeshi la polisi kwa kupita kwenye maeneo yote wanayonunua vyuma chakavu ambapo walianza na eneo la Mji mdogo wa Himo, maeneo ya Holili na Moshi Mjini lakini hawakufanikiwa kuzipata.
Aidha Mhandisi Limbe amesema kipindi cha nyuma pia ziliibiwa mita za maji, baada ya kuanzisha msako walizikuta kwa wafanyabishara ambao hununua vyuma chakavu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Moshi Zephania Sumaye, ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Moshi (MUWSA),kuacha kuweka mita za maji mbali na makazi ya wananchi anayepatiwa huduma hiyo na badala yake wazifunge mita hizo jirani na nyumba.