![]() |
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Abdallah Mwaipaya akizungumza na watumishi wa Ruwasa mkoa wa Kilimanjaro, katika Ukumbi wa Mikutano wa KKKT Mwanga mnamo Mei 21, 2024. (Picha Na. KISENA) |
MWANGA, KILIMANJARO
Serikali Wilaya ya Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro, imewaonya watumishi wa vyombo vya watumia maji ngazi ya jamii (CBWSO) kuacha tabia ya kupita kila nyumba na kukusanya fedha za maji na badala yake ametaka fedha zote zinazotokana na mapato ya serikali kulipwa kwa kutumia mifumo ya GEPG kama ambavyo serikali imelekeza.
Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Abdallah Mwaipaya, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Watumishi wa RUWASA Mkoa wa Kilimanjaro, kilichofanyika wilayani humo na kuhudhuriwa na uongozi wa RUWASA mkoa, mameneja wa RUWASA wa Wilaya pamoja viongozi wa vyombo vya watumia maji.
Alisema Serikali imeweka utaratibu wa namna mapato ya serikali yanavyokusanywa kwa kutumia mifumo ya GEPG, lakini cha kushangaza wako baadhi ya watumishi wamekuwa wakikusanya fedha hizo kwa kupita mitaani bila kufuata utaratibu.
Aidha mkuu huyo wa wilaya alivitaka vyombo vya watumia maji ngazi ya jamii (CBWSOs) vinavyosimamiwa na Wakala ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), kuhakikisha vinasimamia na kuiendesha miradi ya maji ili iweze kutoa huduma hiyo muda wote kama ambavyo imekusudiwa, huku akizitaka CBWSO hizo kujiepusha na kuwabambikizia wananchi bili za maji.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Kilimanjaro Injini Weransari Munisi, alisema lengo la kikao kazi hicho kwa watumishi wa RUWASA ni kutathmini shughuli ambazo wamezifanya kwa kipindi cha Robo Tatu cha kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.
Alisema kikao hicho kitajadili shughuli mbalimbali ambazo wamekuwa wakizitekeleza, kuangalia changamoto wanazokutana nazo wakati wa kutekeleza shughuli hizo na kuona namna ambavyo wanaweza kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo.
Awali akizungumza Kaimu Meneja wa RUWASA Wilayani Mwanga Injinia Samwel Mwakipesile, alisema iko miradi ya maji ambayo inaendelea kutekelezwa ndani ya wilaya hiyo na kwamba kukamilika kwa miradi hiyo itakwenda kuondoa changamoto ya maji kwa wananchi waishio maeneo ya vijijini.
Naye Meneja wa RUWASA Wilaya ya Siha Injinia Emmy George, alisema upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya hiyo kwa sasa umefikia asilimia 83 na kwamba ifikapo mwezi Juni 30 mwaka huu huduma hiyo itafikia asilimia 87.
Tathmini iliyopo kwa sasa katika Mkoa wa Kilimanjaro Wakala ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imefikia Wastani wa upatikanaji wa Maji Safi na Salama kwa maeneo ya Vijijini ni asilimia 83.9 na mpango ifikapo mwaka 2025 huduma hiyo kwa maeneo ya vijijini ni kufikia asilimia 85.