Serikali Mkoa wa Kilimanjaro, imewataka waajiri kutokuwanyima Wafanyakazi wao kujiunga na Vyama vya Wafanyakazi kutokana na ukweli kuwa kujiunga kwao kuna manufaa haswa inapokuja kutetea maslahi yao kazini.
Hayo yamo kwenye taarifa ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu Babu, iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia masuala ya Utawala na Rasilimali watu mkoa wa Kilimanjaro Amos Machilika, wakati wa hafla ya kuwazawadia Wafanyakazi Bora na Wafanyakazi Hodari mkoani humo hafla iliyofanyika katyika ukumbi wa mikutano wa mkuu huyo wa mkoa.
Amesema wako baadhi ya waajiri wamekuwa wakiwatisha Wafanyakazi ambao wameonesha nia ya kujiunga na vyama vya wafanyakazi ikiwemo kuwatisha kuwa watawafukuza kazi, jambo ambalo amesema sio sawa maana ni haki kila mfanyakazi kujiunga na chama cha wafanyakazi chochote anachokipenda ili kutetea maslahi yake pale anapoona mambo hayaendi.
Aidha ametoa wito kwa mamlaka zinazohusika na uteuzi wa wafanyakazi bora na hodari katika vyama vya wafanyakazi kuzingatia vigezo wakati wa kufanya uteuzi huo badala ya kufanya uteuzi wa kimazoea ikiwemo kuteua watu kama hisani ua zawadi.
Vievile amewataka waajiri kuzingatia kanuni zilizoko wakati wa kuitisha vikao vya mabaraza ya wafanyakazi kwani kanuni hizo ziko wazi.
Akiongea wakati wa hafla hiyo Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa wa Kilimanjaro Hassan Kopwe, amesema jumla ya wafanyakazi 450 wametunukiwa vyeti na zawadi mbalimbali kama wafanyakazi bora na hodari kwa mwaka wa 2023, baada ya kuteuliwa na vyama vinavyowakisha maeneo yao ya kazi.
Akizungumzia changamoto zilizoko kwenye uendeshaji wa vyama vya wafanyakazi Kopwe amesema ni pamoja na baadhi ya wafanyakazi kuwazuia wafanyakazi wasijiunge na vyama vya wafanyakazi jambo ambalo amesema hufifisha dhana ya mshikamano miongoni mwa wafanyakazi.
Kuhusu maadhimisho hayo Kopwe amesema utoaji zawadi huo ni mwendelezo wa Sikikuu ya Wafanyakazi iliyofanyika karibuni, ambako Kitaifa ilifanyikia mkoani Arusha.
Naye Katibu wa TUGHE mkoa wa Kilimanjaro Jackson Nyaganilwa amesema Chama cha Wafanyakazi ndicho chombo pekee kinachokusanya maoni ya wafanyakazi na kuzungumza kwa niaba ya Wafanyakazi wote ndani ya nchi.




