BOMANG’OMBE, HAI
Serikali imelipongeza Kanisa la
Tanzania Assemblies Of God (TAG) Gethsemane lililopo Wilayani Hai mkoani
Kilimanjaro kwa namna ambavyo linawajengea watoto wadogo misingi mizuri ya
kumjua Mungu.
Mkuu wa Wilaya ya Hai Amiri
Mkalipa, alitoa pongezi hizo wakati akitoa salamu za Serikali kwenye
maadhimisho ya miaka 85 ya kuanzishwa kwa Kanisa la Tanzania Assemblies
Of God (TAG) hapa nchini.
Hafla ambayo ilienda sambamba na
maadhimisho ya kutimiza miaka 44 ya kuanzishwa kwa Kanisa TAG Gethsemane
lililopo Wilayani humo.
Amesema mambo ambayo yamemfurahisha
wakati amefika kanisani hapo ni namna ambavyo Kanisa la TAG
linavyowajengea misingi ya kuwaandaa watoto wadogo kuja kuwa Watanzania
waliobora na hivyo akawataka wazazi na walezi kuendelea kuwalea watoto wao
katika misingi ya dini, Ili kutengeneza kizazi chenye hofu ya Mungu.
Amesema mzazi bora ni yule
anayemchukua mtoto wake na kwenda naye kanisani kwani atajua madhara ya ukatili
wa kijinsia pamoja na madhara ya ulawiti.
Aidha mkuu wa wilaya ya Hai,
amelipongeza kanisa la TAG kwa na utaratibu wa kujitolea na kwenda kuwasaidia
watoto wenye mahitaji maalum ili kueneza upendo kwa wasio na uwezo kujiona
wako, sanjari na kushiriki shughuli za m upandaji wa miti pamoja na uchangiaji
wa damu.
Awali akizungumza mzee Kiongozi wa
Kanisa la TAG Gethsemane Wilaya ya Hai, Daudi Lekei, amesema katika
kuadhimisha miaka 85 ya TAG nchini, wameshiriki upandaji wa
miti, kufanya usafi wa mazingira katika maeneo yanayozunguka kanisa,
kuchangia damu pamoja na kwenda kutembelea kituo cha watoto yatima na kutoa
misaada mbalimbali ya kibinadamu.
Maadhimisho ya miaka 85 ya kuanzishwa kwa TAG hapa nchini ni kufuata maandiko matakatifu ya Mungu ya kukumbuka na kuyaishi mambo mazuri ya watangulizi katika kuongoza kondoo wa Bwana.
