![]() |
| Mwenyekiti wa Halmashauri ya Moshi DC Morris Makoi. (Picha na. KISENA) |
ARUSHA CHINI, MOSHI
Serikali Kuu imetenga jumla ya Sh milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari katika kijiji cha Mikocheni, Kata ya Arusha Chini, Halmashauri ya wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Ujenzi wa shule hiyo unatarajia kuwaondolea kero wanafunzi wa eneo hilo ambao huwa wanasafiri umbali mrefu kufuata elimu ya sekondari maeneo mengine ikiwemo nje ya mkoa wa Kilimanjaro.
Hayo yameelezwa jana na Mwenyekiti Halmashauri ya Wilaya ya Moshi (MDC), mkoani Kilimanjaro Morris Makoi, wakati alipotembelea eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.
“Ili kufanikisha ujenzi huo, kwa kuanzia Hamashauri ya Wilaya ya Moshi tayari imetenga milioni 250 kutoka mapato yake ya ndani, ambazo zitatumika katika hatua za awali za mradi huo wa ujenzi wa shule mpya ya sekondari”, alisema Makoi.
Pia amesema wako wadau wengine ikiwemo Kampuni ya uzalishaji sukari ya TPC wameonyesha nia ya kutoa michango yao kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.
Akizongea Ofisa mtendaji wa Kiwanda cha uzalishaji wa Sukari cha TPC, anayeshughulikia masuala ya Utawala Jaffari Ally, meisema Kampuni hiyo itajenga madarasa mawili ikiwa ni mchango wa kampuni hiyo katika kujenga shule hiyo mpya.
“Mbali na Kampuni yetu ya TPC, Mimi binafsi ninatoa mchango wangu binafsi wa Sh milioni moja na ni kutokana na umuhimu wa mradi huu katika kukuza elimu”, amesema Ally.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Arusha Chini Leonard Waziri, ametoa mchango wake wa Sh milioni moja, ambapo amesema ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kujenga shule hiyo.
“Shule hii itakuwa na umuhimu mkubwa kwa wakazi wa eneo hili, haswa ikitiliwa maanani watoto wetu wanaohitimu elimu ya msingi hulazimika kutembea umbali wa kati ya kilomita saba kwenda na kurudi shuleni”, amesema Waziri.
Ameongeza “Ukipiga hesabu ni sawa na mtoto anatembea kilomita 14 kwa siku; huu umbali ni mrefu sana; mbali na urefu huo, pia wanafunzi haswa wa kike wanakumbana na changamoto zingine ambazo zinaweza kukatisha mipango ya kupata elimu”, alisema.
