USHIRIKA WA NEEMA, MOSHI
Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Dkt. Fredrick Shoo, amekipongeza Chuo cha Montessori Usharika wa Neema Moshi, kwa kutoa taaluma bora ya elimu ya malezi na makuzi, ambayo imesaidia kuibadilisha jamii.
Dkt. Shoo ameyasema hayo jana, wakati alipotembelea Chuo cha Montessori Usharika wa Neema, kilichopo Manispaa ya Moshi Kilimanjaro, ambapo alipata fursa ya kuzungumza na Wanafunzi pamoja na Wakufunzi na kusisitiza suala la malezi ni suala mtambuka katika jamii ya sasa inayohitaji nguvu ya pamoja.
Kiongozi huyo wa Kiroho alisema kukosekana kwa taaluma ya malezi imechangia kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili kwenye jamii iliyopo kwa sasa na kuwapongeza wanachuo ambao wamekuja kuchukua kozi ya masomo ya malezi na makuzi katika chuo hicho.
Alisema ili kuwa na jamii njema wazazi na walezi, wanatakiwa kuanza kuwalea watoto wao kimaadili wakiwa msingi jambo ambalo litasaidia kuondokana na tatizo la mmonyoko wa maadili katika jamii.
Aidha Askofu Dkt. Shoo aliwataka wanachuo ambao wanaochukua kozi ya masomo ya malezi na makuzi katika chuo cha Montessori, wahakikishe kwamba watakapohitimu elimu hiyo, waweze kwenda kuifundisha jamii kuhusu misingi ya malezi bora ili kuwa na jamii yenye afya njema na maadili katika jamii.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Montessori Ushirika wa Neema Moshi, Sister Christine Nakey, alisema tangu kuanzishwa kwa kozi hiyo yako mafanikio makubwa, wanafunzi wamebadilika kitabia pindi wanapojifunza wamekuwa wakipata maarifa na taaluma bora inayowasaidia kuja kuwa walezi bora katika jamii.
Aidha alisema bado jamii inahitaji mafunzo kama haya ya malezi na makuzi kwa mtoto kwani sio kila mmoja anaweza kuwa na taaluma hiyo.
Alisema wanafunzi wengi waliopitia katika chuo hicho cha Mntessori Usharika wa Neema,wamekuwa baraka kubwa katika jamii na watoto wengi wameweza kusaidika, kujengwa kinidhamu, kimaadili na kuwa na nidhamu bora.
Naye Mkufunzi katika chuo hicho Marco Alfred, alitoa wito kwa wazazi na walezi kutumia fursa Chuo hicho cha Montessori, kuwaleta vijana wao mbalimbali ili waweze kupata elimu inayotolewa na chuo hicho.










