MOSHI, KILIMANJARO
Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro, imetakiwa kuzisimamia kikamilifu sheria ndogo ambazo zimetungwa na Manispaa hiyo, ambazo zitawezesha atakayekamatwa akitupa takataka hovyo pamoja na kuchafua mazingira kutozwa faini ya isiyopungua Sh elfu 50 kama ilivyokuwa zamani.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, ametoa kauli hiyo hivi karibuni, wakati wa zoezi la uzinduzi wa gari jipya la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lenye uwezo wa kubeba Lita 500,000 na madawa Lita 300,000 hafla iliyofanyika katika Ofisi za Jeshi hilo mkoani.
Amesema kuwa kuna changamoto za wananchi kutupa takataka hovyo barabarani, kwenye mifereji ya maji machafu na kuzitelekeza taka hizo ambazo zimekuwa zikichafua mazingira na kumtaka Mkuu wa Wilaya ya Moshi Zephania Sumaye kuhakikisha kwamba anawapanga Maaskari wa Jeshi la Akiba ili kuwafuatilia watu wote watakaobainika kutupa taka wanakamatwa na kutozwa Sh elfu 50.
Katika hatua nyingine Babu, amemuagiza mkuu wa Wilaya ya Moshi kupanga ziara ya kutembelea Standi kuu ya mabasi Moshi na kuzungumza na maajenti wa mabasi ili kila basi,liweze kuwa na chombo cha kutupia takataka na abiria atakayeonekana akitupa takataka nje ya basi hilo basi hilo litakamatwa na litatozwa faini.
Aidha amepiga marufuku wananchi wote kutupa takataka na kuchafua mazingira hovyo ili kuendelea kuyaweka mazingira ya mji wa Moshi kuwa masafi na kuepuka kukumbana na magonjwa ya mlipuko.
Amesema wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro wanatakiwa kuzingatia kutotupa takataka hovyo kuanzia kwenye magari, nyumbani na kwa wanannchi wanaotembea kwa miguu ili kuuweka mji safi na kuwa mkoa wenye mazingira bora.
Alisema lengo lake ni kuhakikisha kuwa mkoa wa Kilimanjaro unashika namba moja kwa kuwa na mazingira bora na masafi na kuongoza kwa usafi kitaifa kama ambavyo ilikuwa miaka ya nyuma.
Kwa upande wake Ofisa Mazingira MAnispaa ya Moshi alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu ya usafi wa mazingira kwa wananchi wote ili wajue umuhimu wa kutunza mazingira yanayowazunguka.
Alisema wanancvhi wanatakiwa kuendelea kulipa ada ya taka ili kuviwezesha vikundi vya usafi kuendelea kufanya usafi na kutunz mazingira vizuri ya Manispaa hioyo.