Dr. Subi awataka wananchi kujenga tabia ya kupima Afya zao mara kwa mara

Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi (Kibong’oto) Dkt. Leonard Subi, akizungumza na wakazi wa Sanya waliofika katika Huduma ya Kupima bure iliyoendeshwa na Chama cha Wauguzi Tanzania (TANA) Mkoa wa Kilimanjaro mnamo Mei 21, 2024. (Picha Na. KISENA)

SIHA-KILIMANJARO

Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi (Kibong’oto) Dkt. Leonard Subi, amewasisitiza Wananchi, kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara kwa kuwa wengi hufikiri wana afya njema wawapo majumbani jambo ambalo sio kweli.

Mkurugenzi wa hospitali hiyo Dkt. Subi aliyasema hayo Mei 21, 2024, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupima afya bure kwa wananchi wa wilaya hiyo, kamepeni ambayo inaendeshwa kwa siku tatu na Chama cha Wauguzi Tanzania TANA kwa kushirikiana na wataalamu wa afya kutoka Kibong’oto pamoja na wataalamu wa hospitali ya Wilaya ya Siha, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani kwa mkoa wa Kilimanjaro.

Dkt. Subi alisema lengo la kampeni hiyo ni kusogeza huduma karibu kwa wananchi ili kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kupima afya zao pamoja na kupatiwa elimu, uchangiaji wa damu, saratani ya mlango wa kizazi , saratani ya matiti, kisukari,  pamoja na huduma za upimaji wa ugonjwa wa Kifua Kikuu.

Mkurugenzi huyo alisema watu wengi wamekuwa wakikaa majumbani, wanajiona wapo sawa,  lakini kwa uhalisia wanakuwa na changamoto za kiafya.

 “Sisi kama Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi (Kibong’oto) tumekuja hapa kusogeza huduma za  afya kwa wananchi ili kuwawezesha kupima afya, kutoa elimu, pamoja na wao kuweza kuchangia damu,’’alisema.

Awali akizungumza Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi Tanzania Mkoa wa Kilimanjaro (TANA) Pendo Shayo, alisema kuwa lengo la kuanzisha Kampeni hiyo ya uchunguzi wa afya mashuleni ni kuwajengea wanafunzi tabia ya kupima afya zao ili kujenga taifa la watu wenye kujali afya zao hapo baadaye.

Akizundua Kampeni hiyo Mkuu wa Wilaya ya Siha Dkt, Christopher Timbuka, amewapongeza wauguzi wote katika mkoa wa Kilimanjaro kwa kuanzisha kampeni ya kupima afya sanmbamba na kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia mashuleni,

Mkazi wa Siha Happiness Kileo, mwananchi aliyejitokeza kupata huduma ya upimaji wa afya, amesema amefurahishwa na huduma nzuri alizozipata mahali hapo kwa kuwa amepata nafasi ya kupima shinikizo la damu, ugonjwa wa kisukari, hivyo amefurahishwa na huduma hizo.

Mkazi mwingine wa Siha David, ameishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na kusema kuwa jambo hilo lina tija kwa jamii kwa kuwa mtu unaweza ukawa unaishi ukidhani uko salama lakini kumbe una changamoto za kiafya.

“Naishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuiletea vifaa tiba hospitali ya Kibong;oto vifaa ambavyo vimetuwezesha sisi wananchi kuweza kutufikia na kuweza kupimwa bure bila kulipia.




 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.