TRITA-MOSHI, KILIMANJARO
Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda Moshi Mkoa wa Kilimanjaro (TRITA), kimetoa mafunzo yahusuyo masuala ya Uhamiaji kwa taasisi mbalimbali zikiwemo za umma na binafsi zilizopo hapa nchini.
Mwaka 2018 TRITA ilianzisha Programu za mafunzo ya masuala ya ki-uhamiaji kwa taasisi mbalimbali hapa nchini, yaliyokuwa na lengo la kushirikisha wadau katika kusimamia masuala ya uhamiaji kwenye taasisi za umma zilizoajiri wageni kutoka nje na taasisi ambazo hazijaajiri wageni.
Awali akizungumza Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda Moshi (TRITA) Mrakibu Msaidizi Dkt. Husein Namkambe, amesema kozi hizo zimeleta mafanikio chanya ya kiutendaji, yakiwemo mabadiliko ya Sheria.
“Kuna masuala kadhaa yamepatikana kama mafanikio, mojawapo ni uweko wa mabadiliko ya Sheria katika utoaji wa vibali vya kusafiria, haya yote ni matokeo ya kozi hizi tunazoendelea nazo kuzitoa, kutokana na kuchukua maoni ya wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakihudhiuria kozi hizi”,alisema Mrakibu Namkambe.
Vile vile alisema mafanikio mengine ni kuweko kwa ushirikiano kupitia idara na wadau wake, umekuwa uko karibu zaidi kuliko ilivyokuwa awali kabla ya kuanza kutoa kozi hizo.
Aidha Dkt. Namkambe amesema fanikio la tatu ni kwamba wamekuwa wakichukua maoni ya wadau na wakati mwingine yamesaidia kuboresha huduma ya TRITA.
Akizfunga mafunzo hayo ya siku tano, yaliyofanyika katika ukumbi wa chuo hicho Mkuu wa wilaya ya Moshi Zephania Sumaye, aliwataka wahitimu hao, kwenda kutekeleza kwa vitendo yale yote waliyofundishwa juu ya masuala ya Ki-Uhamiaji.
“Naomba kutoa maelekezo kwenu TRITA yale ambayo wadau hawa wameyatoa kama changamoto kwao, msiyachukue na kwenda kuyaweka kwenye makabati, nendeni mkayafanie kazi na kuyaboresha zaidi hususani masuala mazima ya ulinzi ,”alisema DC Sumaye.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake Mshauri wa masuala ya Sheria na mambo ya Utawala Casim Msimbo na Ofisa Rasilimali watu kutoka Kampuni ya Madini GGM Cesilia Kanabo, walisema, elimu waliyoipata itakwenda kuwa chachu katika utendaji kazi wa majukumu yao.
“Kwa mafunzo haya tuliyoyapata ya siku tano, yatakwenda kuwa chachu na tija kwa kazi zetu za kila siku,”walisema washiriki wa mafunzo hayo.
Naye Kamanda wa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro Mrakibu Mwandamiizi Fahik Nyakunga, alisema changamoto ya Uhamiaji haramu mkoani humo, imeendelea kupungua kutokana na kuweko kwa ushirikiano mzuri kati yao na wadau mbalimbali.
“Takwimu za wageni wanaoingia kupitia vipenyo, vimepungua kwa sababu tunashirikiana kwa pamoja katika kudhibiti.”
Alisema takwimu za vituo vya kuingia kwenye mipaka ya Holili, Tarakea na kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA) zimeongezeka na hii inaonesha kwamba, wageni wanazidi kuongezeka kuja nchini kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za kiuwekezaji”, alisema Mrakibu Nyakunga.
Pia alisema Jeshi la Uhamiaji mkoani humo, linaendelea na Kampeni yake ya MJUE JIRANI YAKO! ambayo inawashirikisha viongozi mbalimbali kuanzia ngazi za Mitaa, Vitongoji, Vijijini na Kata, kutoa taarifa sehemu yoyote ambayo wataona kuna wageni wanaoingia katika maeneo yao na hawawafahamu vizuri ili waweze kudhibitiwa.
Mafunzo hayo yaliyotolewa na TRITA kwa wadau mbalimbali hapa nchini, yaliambatana na Utalii wa Ndani kwa washiriki wa kozi hiyo kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro KINAPA.