MWANGA- KILIMANJARO.
Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro, umefanya Mkutano Mkuu wa Pili wa Mwaka wa Wilaya kwa Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii kwa ajili ya kujadili uelewa, kutathmini na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maji na usafi wa mazingira.
Mkutano huo ambao umefanyika Mei 24,2024 katika ukumbi wa mikutano wa makao makuu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT Wilayani humo na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa maji na usafi wa mazingira Wilayani Mwanga.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilayani humo, Meneja wa (RUWASA) Wilayani humo Injinia Christine Kessy amesema huduma ya maji kwa maeneo ya Mwanga vijijini inapatikana kupitia vyanzo mbalimbali vya maji hususani chenicheni, mito, visima virefu na vifupi pamoja na uvunaji wa maji ya mvua.
Amesema Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Wilaya ya Mwanga ina wakazi wapatao 148,763 ambapo watu 125,568 wanaishi maeneo ya vijijini, huku wakaazi waishio maeneo ya vijijini 98,366 wanapata huduma ya maji safi na salama ambao ni sawa na asilimia 78.33 ya wakazi wote waishio maeneo ya vijijini.
Amesema RUWASA Wilaya ya Mwanga imejipanga kuondoa kero ya maji vijijini kwa kufanya utafiti wa vyanzo vipya vya maji, usanifu wa miradi mipya ya maji, ukarabati na upanuzi wa miradi ya maji iliyopo na kujenga miradi mipya ili kutimiza azima na malengo ya serikali pamoja na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kufikisha lengo la asilimia 85 ya usambazaji wa maji vijijini.
Akifungua Mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Abdallah Mwaipaya, amesema mwaka wa fedha 2023/2024 Wilaya hiyo, ilipokea fedha takribani Sh bilioni 2.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji huku mwaka wa fedha ujao 2024/2025 RUWASA Wilayani humo kwenye bajeti hiyo wametenga kiasi cha Sh bilioni 2.3 ambazo zitakwenda kutekeleza miradi ya Maji Safi na Salama.
Katika hatua nyinmgine Mkuu huyo wa Wilaya amepiga marufuku kwa Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO) kukusanya pesa au kupokea pesa taslimu kutoka kwa wananchi na badala yake wananchi wanatakiwa kulipa fedha hizo kwa kutumia mifumo ya serikali ya GEPG.