KIBAHA, PWANI
Manispaa ya Moshi imeshika nafasi ya pili nchini Tanzania katika
tuzo za Halmashauri bora katika Afya na Usafi wa Mazingira inayotolewa na Wizara
ya Afya ili kuongeza tija na ushindani kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo Mstahiki Meya wa
Manispaa ya Moshi Injinia Zuberi Kidumo amesema mwaka huu wamepanda nafasi moja
baada ya mwaka 2022-2023 kushika nafasi ya tatu
“Tunashukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuwa washindi wa
pili hizi ni jitihada kubwa mwaka jana Manispaa ya Moshi tulikuwa washindi wa
nafasi ya tatu na mwaka huu tumesogea na kuwa washindi wa pili,” amesema
Injinia Kidumo.
Manispaa ya Moshi ni miongoni mwa Manispaa nchini ambazo
zimekuwa katika kinyang’anyiro hicho kwa muda mrefu ambapo Injinia Kidumo
ameweka bayana mikakati ya kuirudisha Moshi kuwa ya mfano katika kategori hiyo.
“Nafasi ya Kwanza imechukuliwa na Manispaa ya Shinyanga. Bado
tunaendelea kupambana ili tuweze kushika katika nafasi ya kwanza kama zamani. Haya
ni mashindano, sisi tukiwa tunapambana kuendeleea kutetea nafasi yetu ukae
ukijua kwamba kuna mwenzako naye anapambana kuitaka hiyo nafassi ya kwanza
anaboresha kwake,” ameongeza Mstahiki Meya huyo.
“Mikakati; ni kuhakikisha tunakwenda kuboresha zaidi maeneo
yetu, taka zinakuwa ni changamoto kubwa sana kutokana na kila siku ya mungu
familia zinaongezeka , familia mpya maeneo”, amesema Injinia Kidumo
Makamu wa Rais Dk. Philip Isdori Mpango, ametoa tuzo hizo akiwa sambamba na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu na kuwakabidhi Manispaa na Halmashauri washindi katika hafla iliyofanyika Kibaha, mkoani Pwani.
Kwa upande wa Halmashauri ya Moshi imejinyakulia tuzo ya hospitali
ya bora baada ya Hospitali ya Kibosho kushika nafasi ya Pili kwa utoaji wa
huduma kwa wagonjwa.
