Kamati ya Maafa Moshi kutoa Magodoro 20 waathirika mafuriko Arusha Chini


ARUSHA CHINI, MOSHI

Mwenyekiti wa Kamati ya maafa Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro Zephania Sumaye, amesema kamati hiyo itatoa magodoro 20 kwa ajili ya wahanga wa mafuriko hayo walioko Kata ya Arusha Chini.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti huyo Mjumbe wa Kamati hiyo Moris ameyasema hayo jana,wakati akipokea msaada wa tani moja ya unga wa sembe, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi, iliyotolewa na Diwani wa Kata ya Arusha Chini Leonard Waziri.

Makoi amesema hadi sasa kuna wahanga 487 kati yao 418 wamehifadhiwa na ndugu zao huku wengine 69 bado wanaendelea kuishi kwenye kambi maalum ambazo zimetengwa na serikali.

“Kati ya wahanga hawa 487, wahanga 69 ndiyo wanaishi kambini kutokana na kukosa kabisa mahali pa kuishi huku wengine waliobakia wakiwa wamehifadhiwa kwa ndugu na jamaa zao”, alisema.

Alisema wahanga hao wamekosa makazi ya uhakika baada ya nyumba zaidi ya 137 kuzolewa na maji yaliyosababishwa na mafuriko kufuatia mvua zinazooendelea kunyesha mkoani Kilimanjaro.

Makoi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi (MDC) ametoa mchango wake wa kilo 500 za unga pamoja na neti 60 kwa ajili ya wahanga walioko kwenye kambi zilizoko kwenye Kanisa Katoliki Mikocheni, Taasisi ya FT-Kilimanjaro, jengo la wavuvi lililoko Mikocheni na kwenye Zahanati iliyoko eneo la Mikocheni.

Kwa upande wake diwani wa Kata ya Arusha Chini Leonard Waziri, alikabidi msaada wa tani moja ya unga wa sembe kwa waathirika wa mafuriko waliowekwa kambi mbalimbali katika kijiji cha Mikocheni kilichopo katika kata hiyo na kusema kuwa tayari serikali inaendelea kuangalia jinsi ya kushughulikia hatma zao.

Naye Diwani wa Kata ya Old Moshi Mashariki Jane Mandara, alikabidhi nguo na viatu kwa wahanga hao.

Akizungumza diwani wa Kata ya Mbokomu Raphael Materu, aliwasisitiza viongozi kusimamia vizuri misaada yote inayotolewa na wadau malimbali, ili iwafikie walengwa wote .

Viongozi wengine waliowatembelea wahanga hao kwa siku ya Ijumaa ya Mei 10, 2024 ni pamoja na Diwani wa Kata ya Mwika Kaskazini Samuel Shayo, Ally Badi, Fabiola Massawe, Delis Mosha, Miliam Msoka, na Delina Temba.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.