KIBONG'OTO, SIHA-KILIMANJARO
Jumuiya ya Ulaya inayosimamia mambo ya Utafiti (EDCTP) imeichagua Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi (Kibong’oto) kusimamia tafiti na ugunduzi wa dawa mpya za kupunguza matibabu ya Kifua Kikuu Sugu kutoka miezi sita hadi miezi minne au chini ya hapo.
Hayo yalibainishwa na Kaimu Mkuu wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ushauri Dk. Alphonce Liyoyo, wakati akitoa taarifa ya miaka 98 tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo mwaka 1926 kwa waandishi wa habari mkoa wa Kilimanjaro waliotembelea hospitali hiyo.
Alisema baada ya hospitali hiyo, kusimamia tafiti za kisayansi pamoja na ugunduzi wa dawa mpya za kupunguiza matibabu kwa wagonjwa wa Kifua Kikuu Sugu kutoka kutumia miezi sita hadi miezi minne, Jumuiya ya Ulaya inayosimamia mambo ya Utafiti (EDCTP) imeweza kuichagua hospitali ya Kibong’oto kuzisimamia nchi zingine tatu ikiwemo nchi ya Gabone, Malawi na Msumbiji.
“Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi (Kibong’oto) ndiyo hospitali pekee iliyopewa dhamana na Jumuiya ya Ulaya inayosimamia mambo ya Utafiti (EDCTP) kutokana na uzoefu na uwezo, iliyoonesha katika kufanya tafiti mbalimbali ambazo inazisimamia katika kufanya utafiti hizo na uchunguzi ambao unafanyika kwa kushirikiana na Serikali ya Umoja wa Ulaya (UN).”alisema Dk. Liyoyo.
Pia alisema Hospitali ya Kibong’oto inaongoza kwa kufanya tafiti ambazo zimesaidia matibabu kwa wagonjwa wa Kifua Kikuu Sugu waliopona, baada ya kuruhusiwa kurudi nyumbani lakini bado wamekuwa wakipata changamoto kwenye sehemu ya mapafu yao.
“Tumekuwa na mpango maalumu wa kuwafuatilia wagonjwa wa Kifua Kikuu Sugu waliopona na kuruhusiiwa kurudi nyumbani, ziko changamoto zingine ambazo zimekuwa zikiwapata kutokana na mapafu yao yalikwisha kuharibika, tumekuwa tukiwafuata huko waliko na kuwapatia matibabu, ili kuhakikisha kwamba mapafu yao yanafanyiwa mazoezi ili kuwasaidia waweze kuendelea kuishi.
Alisema “Mpango huu unasimamiwa na Hospitali ya Kibong’oto ambapo inafanya kazi katika nchi tatu za Uganda, Malawi na Kenya,”alisema Dk. Liyoyo.
Aliongeza kuwa “Yako mafanikio mengi ambayo yamepatikana katika kipindi hiki cha miaka 98 tangu kuanzishwa kwa hospitali ya Kibong’oto, ikiwemo kuondoa matumizi ya sindano kwa wagonjwa wa Kifua Kikuu Sugu, ambao walikuwa wanatibiwa, kupitia tafiti ambazo zilifanyika katika hospitali yetu tuliweza kuwezesha kuondolewa kwa adha ya hiyo kwa waginjwa kuchomwa sindano, ambapo kwa sasa wagonjwa wa Kifua Kikuu Sugu wanatumia vidonge peke .
Aidha alisema Kibong’oto imeweza kusaidiana na serikali kuweka muongozo wa uchunguzi wa Kifua Kikuu Sugu kwa wagonjwa wanaohisiwa kuwa na Kifua Kikuu ambapo kwa sasa ugonjwa wa kisukari wameingizwa kwenye muongoz huo.
“Wagonjwa wanaohisiwa kuwa na Kifua Kikuu Sugu wanapotakiwa kuchunguzwa wachunguzwe na uwepo wa ugonjwa wa kisukari kwa kuwa imeonesha kati ya magonjwa nyemelezi ambayo yanawapata wagonjwa wengi wa Kifua Kikuu nchi asilimia kubwa pia ni wagonjwa wenye maambukizi ya kisukari.
Alisema kwa sasa muongozo huo unawataka kuchunguzwa na ugonjwa wa kisukari, hiyo ni kutokana na tafiti zilizofanyika katika hospitali ya Kibong’oto.
