Tani moja ya saruji yatolewa waathirika wa mafuriko Mbokomu



MBOKOMU, MOSHI VIJIJINI

Diwani wa Kata ya Mbokomu Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro Raphael Materu, ametoa msaada wa tani moja ya mifuko ya saruji kwa familia ya Peter Kimambo, iliyopoteza mtoto wao, baada ya kuangukiwa na nyumba na kupoteza maisha huku nyumba ya wazazi wake ikisombwa na mafuriko yaliyotokea Aprili 24 mwaka huu.

Akitoa salama za rambirambi kwa familia hiyo, baada ya maziko kufanyika, alisema kutokana na changamoto iliyotokea katika familia hiyo, anatoa msaada wa tani moja ya saruji yenye thamani ya Sh 400,000, ili familia hiyo iweze kuanza ujenzi wa nyumba mpya.

Alisema baada ya mafuriko hayo kutokea yaliweza kusababisha familia hiyo kukosa makazi na kukabiliwa na changamoto kubwa katika ujenzi wa nyumba yao iliyosombwa na maji pamoja na huduma zingine za kijamii.

Akizungumzia athari za mafuriko zilizosababishwa na mvua hizo katika kata hiyo amesema, baadhi ya miundombinu ikiwemo ya maji na barabara imeathirika kwa kiasi kikubwa na hivyo kusababisha wananchi wa kata hiyo kukosa  huduma ya maji safi na salama kwa takribani wiki.

Aidha alisema vipo baadhi ya vyanzo vya maji ambavyo walikuwa wakivitegemea kwenda kuchota maji vimefukiwa na udongo huku vingine vikiendelea kubaki licha ya wananchi wanashindwa kufika katika maeneo hayo kwa kuhofia kuangukiwa na ngema.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Moris Makoi, alitoa pole kwa familia hiyo kwa kuchangia kiasi cha Sh 500, 000 ili kuunga mkono, ujenzi wa nyumba hiyo huku mdau wa maendeleo Ebeneza Mringa akichangia kiasi cha Sh 75,000, na Group la Kyaroni Maendeleo wakichangia kiasi cha 150,000.

Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya familia Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Fukeni Kanisa la (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Robinson Moshi, alimshukuru Mbunge, Mwenyekiti wa halmashauri, diwani na wadau wengine walioguswa na kuishika mkono familia hiyo kutokana na mazingira magumu wanayoishi kwasasa kutokana na kuharibiwa makazi yao pamoja na mazao.

Diwani wa Kata ya Mbokomu Raphael Materu akizungumza jambo wakati akitoa taarifa ya mafuriko katika kata yake kwa waandishi wa Habari mnamo Aprili 25, 2024.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.