Chadema yasisitiza watanzania kujiandikisha Kidijitali

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewasihi wanachama na wapenzi wa chama hicho kuweka nguvu ya pamoja katika kukiimarisha chama hicho sambamba na kujiandikisha kwa njia ya Kidigital nchi nzima, kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu pamoja na uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2025.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara Benson Kigaila, aliyasema hayo Aprili 30 mwaka huu mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mashujaa ulioenda sambamba na matembezi ya Amani.

Kigaila alisema chama hicho kimeanzisha kampeni ya kupita nyumba hadi nyumba ili kupata wafuasi watakaokiwezesha chama hicho kupata ushindi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2025.

Aidha alisema ili kupata viongozi bora Chadema kinataka kuwe na Tume Huru ya Uchaguzi pamoja na Katiba Mpya, ili chaguzi za mwaka huu na ule wa mwaka 2025 ziweze kufanyike kwa haki na zisitoke hujuma kama zilizotokea katika chaguzi zilizopita.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema Taifa Freeman Mbowe, alisema kupatikana kwa Katiba Mpya kutasaidia kuondoa changamoto ndogo ndogo zilizopo kwa sasa nchini.

Alisema Katiba ya sasa inapaswa kubadilishwa au kufanyiwa marekebisho ili kupisha uchaguzi, kwani katiba iliyopo kwa sasa inampa Mamlaka makubwa Rais hasa kwa Viongozi ambao wanasimamia uchaguzi hivyo kuweka mazingira magumu katika chaguzi kwa vyama vingine vya kisiasa.

“Tunaposema tunataka tuandike Katiba Mpya, kama Chadema tunamaono ya kuipeleka nchi katika nchi ya ahadi, tunataka tuondoe kero mbalimbali  zinazowakabili wananchi wanyonge ,”alisema Mbowe.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (BAWACHA) Grace Kiwelu, aliwataka wananchi wa Chadema  kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwa kuwa ni haki yao ya msingi.

“Tunaamini kama mtajitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongopzi kwenye chaguzi za Serikali za vijiji, vitongoji na mitaa, mwaka 2025 utakuwa ni wakati wetu wa kuoingoza nchi.

Alisema mwaka 2025 utakuwa ni mwaka wa uchaguzi mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais, Chadema tunasema sasa ni wakati wetu wa kuonesha njia katika kuiongoza nchi ya Tanzanaia.

Akizungumza Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Moshi Mjini na Meya Mstaafu wa Manispa ya Moshi Raymond Mboya, alisema ikitengenezwa Katiba Mpya kila kitu kitakuwa wazi katika chaguzi zote zijazo.

“Chadema pia tunataka kuwa na watu ndani ya Tume Huru, wawepo watu wa vyama vyote  ili uchaguzi wa Serikali za Mitaa ufanyike kwa haki,  ili kama mtu amekosa kura aweze kuona kweli amekosa kihalali.”alisema Mboya.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.