ARUSHA CHINI/MABOGINI; MOSHI
Wanafunzi wa kike 300 wa Shule za Sekondari Mpirani, Oria, Mabogini na TPC zilizoko Kata ya Arusha Chini na Kata ya Mabogini Halmashauri ya Wilayani Moshi, wamekabidhiwa baiskeli na Shirika lisilo la Kiserikali la ABC IMPACT ili kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shule.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wakipokea baiskeli hizo wanafunzi wa shule hizo akiwemo Mohammed Mstapha kutoka shule ya sekondari Oria, Jesca Tesha na Aureria Kokusima kutoka shule ya sekondari Mpirani;
Walieleza kuwa baiskeli hizo zitawasaidia kupunguza changamoto ya kutembea umbali mrefu kwenda shule ambao umekua ukidumaza kiwango cha elimu na kuwafanya wakutane na madhara mbalimbali ikiwemo kuchelewa shule.
Walisema baiskeli hio zitawasaidia kwa kiasi kikubwa kuepuka changamoto kwani wataweza kuwahi vipindi kwa wakati shuleni pamoja na kupata muda wa kujisomea.
Kwa upande wake Ofisa Elimu Kata ya Mabogini John Mariki, alisema kuwa mradi wa baiskeli kwa watoto wa kike umekuwa chachu kubwa ya maendeleo kitaaluma, kwani baiskeli hizo zimekuwa zikiwasaidia kufika shuleni kwa wakati.
Mariki alisema watoto wa kike wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi katika masomo yao pindi wanapotoka nyumbani kwenda shuleni lakini pia hata wakati wa kurudi nyumbani wamekuwa wakikutana na vishawishi vingi.
Akizungumzia mpango huo Makamu Mkuu wa shule ya sekondari Mpirani Remmy Kaganda aliishukuru taasisi ya ABC IMPACT kwa mradi wao wa Back to school ambao umeleta tija kubwa sana katika shule hiyo.
“Baiskeli hizi zimewasaidia wanafunzi kufika shuleni kwa wakati kwani hata mjongeo chanya katika matokeo kwa wasichana kwa kidato cha nne na kidato cha pili yamezidi kuoneka shuleni hapo.”alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo ya ugawaji wa baiskelui 60 kwa wanafunzi wa shule hizo Mkurugenzi wa Shirika la ABC IMPACT Ayana Kimaro, alisema kutokana na changamoto inayowakabili watoto wa kike ya kutembea umbali mrefu wameguswa kuwapatia baiskeli hizo ili ziweze kuwasaidia kuwahi masomo shuleni.
“Mradi wa Back to School unatekelezwa katika mikoa minne ambayo ni Shinyanga, Dodoma, Arusha na Kilimanjaro, ambapo kwa mwaka huu tunagawa baiskeli 300 kwa awamu ya kwanza katika mkoa wa Kilimanjaro, ikiwemo Kata ya Mabogini iliyoko Wilaya ya Moshi kutokana na wasichana kupitia changamoto ya kutembea umbali mrefu kufika shuleni.







