Prof. Ndakidemi atembelea wahanga wa mafuriko Mabogini, Arusha Chini atoa tani moja ya mahindi

Mbunge wa Jimbo la moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi akikabidhi msaada wa mahindi kwa waathirika wa mafuriko katika Kata ya Mabogini na Arusha Chini hivi karibuni. (Picha na KISENA)


MABOGINI, MOSHI VIJIJINI

Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Mkoani Kilimanjaro Profesa Patrick Ndakidemi, ametoa msaada wa tani moja ya mahindi kwa wahanga waliokumbwa na mafuriko katika Kata ya Mabogini na kata ya Arusha Chini zilizoko Halmashauri ya Moshi mkoani humo, ambao nyumba  na mazao yao yameathirika kwa mafuriko.

Aprili 25 mwaka huu, mafuriko yalitokea kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha mkoani humo,  hususani katika maeneo ya ukanda wa juu na kusababisha maji hayo kuteremka kuelekea upande wa tambarare ziliko kata za Mabogini na Arusha Chini.

Ndakidemi, alitoa msaada huo jana wa tani moja za mahindi ambapo kila kitongoji kilipata magunia 10 ya mahindi, mara baada ya kutembelea vitongoji vilivyoathirika na mafuriko vya Mabogini Juu na kitongoji cha Harusini  vilivyopo katika kata hizo.

Alisema anaendelea kushughulikia suala hilo serikalini ili kuona namna ambavyo wananachi hao wanaendelea kupata misaada mingine kutokana na waathirika hao kutofautiana uhitaji.

“Leo Mwenyekiti wa Kijiji nimekuletea tani moja ya mahindi  naomba tugawane kidogo  wakati Serikali inajiandaa kuja na mambo mengine, nafahamu kuna mazao ya mahindi yaliyokuwa shambani yaliyoharibiwa na mafuriko kwa kidogo hiki naomba mpokee ili wananchi hawa waweze kupata unga wa kula,” alisema Mbunge Ndakidemi.

Aidha alisema anaendelea kupambana Serikali kama kutakuwa na misaaada mingine itakayotolewa  ataileta, kwani tayari suala hilo alisha lifikisha serikalini kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, ambapo kuna mchakato ambao unaendelea wa kiserikali wa kuja kuwaona.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliokabidhiwa msaada huo walimshukuru Mbunge na kumuomba aendelee kuwakumbuka katika upande wa nguo na magodoro.

“Tunamshukuru sana Mbunge wetu Patrick Ndakidemi, kwa kututembelea na kuja kutusaidi, tunakuomba pia utukumbuke na magodoro, mashuka na mablanketi hatuna kabisa, tuna lala chini ya sakafu hatuna cha kujifunika,”walisema.

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mikocheni Salehe Kulakwa, alisema wanaendelea kushirikiana na wenyeviti wa vitongoji jirani kwa karibu zaidi ili kuona wananchi walioathirwa na mafuriko wanaendelea kusaidiwa.

Akizungumza Diwani wa Kata ya Mabogini Halmashauri ya Moshi Dk. Bibiana Massawe, alimshukuru Mbunge Ndakidemi kwa msaada huo alioutoa kwa wahanga wa mafuriko hayo na kuwaomba wadau wengine kuendelea kutoa msaada kwa wahanga hao wa mafuriko kwa kuwa bado wana mahitaji mengi ambayo wanatakiwa kusaidiwa kutokana na kupoteza asilimia kubwa ya mali zao ambazo walikuwa wanamiliki kabla ya kukumbwa na mafuriko hayo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.