Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia ujenzi wa soko la Mbuyuni lilloungua hivi karibuni uendelee, ambapo tayari mamlaka husika ikiwemo TAMISEMI na Wizara ya Fedha zimesha idhinisha fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi huo.
Hayo yameelezwa na jana
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro Injinia Zuberi Kidumo,
wakati akizungumza na wafanyabiashara mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kikao cha
Mkuu wa Wilaya ya Moshi Zephania Sumaye alichokiitisha kwa ajili ya kusikiliza
kero za wananchi.
“Wakati soko lilipoungua tulikuja
kwenye soko hili, kuwajulisha ya kuwa litajengwa upya na kukamilika ndani ya
miezi miwili; Baraza la Madiwani tulikaa tukakubaliana ya kuwa kila Kata
isitishe mradi mmoja ili fedha za mradi huo zitumike kujenga soko ili
wafanyabiashara wasikose mahali pa kufanyia kazi”, alisema Injinia Kidumo.
“Sisi kama Baraza tulishakamilisha
taratibu zote lakini kwa vile taratibu zingine zinatutaka kuomba kibali
TAMISEMI na kile cha kutoka Wizara ya Fedha ili kuidhinishiwa mabadiliko ya
matumizi ya fedha za miradi na ndicho kilichochelewesha kuanza ujenzi wa soko”,
alisema.
Aliongeza, “Niwajulishe ya
kuwa Rais Samia Suluhu Hassan, ameingilia kati swala hilo na leo ametoa idhini
mabadiliko ya matumizi ya fehda hizo kama tulivyoomba na ujenzi unatarajiwa
kuanza ndani ya wiki mbili zijazo”, alisema.
Katika hatua nyingine, Meya
Kidumo amewapongeza Wanawake kwa kuwa mstari wa mbele katika kurudisha kwa
wakati fedha walizokopa ikiwa ni sehemu ya mikopo inayotolewa na halmashauri ya
Manispaa ya Moshi.
Aidha ametoa rai kwa maafisa
wasafirishaji wa bajaj na bodaboda kujiunga na SACCOS ili kupata huduma ya mikopo
nafuu ili waondokane na adha ya kupata mikopo ambayo inakuwa ni vigumu
kuirejesha na hivyo kupelekea wao kunyang’anywa zana zao za kazi.
Akijibu maswali kutoka kwa
Wafanyabiashara hao, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi
Mwajuma Nasombe, amesema tayari halmashauri hiyo imetenga jumla ya snhilingi
bilioni 1.5 kwa ajili ya mikopo ya wanawake, watu wenye ulemavu na vijana.
“Kama mnavyojua mikopo hii ilisitishwa kwa muda; utaratibu wa kutoa mikopo hiyo utakaporudishwa, jitokezeni kwa wingi kuja kukopa maana tayari sisi kama halmashauri tushatenga fedha kwa ajili hiyo”, alisema.
Akijibu changamoto iliyowasilishwa na wafanyabiashara wa soko la mitumba la Meimoria, kuhusu changamoto ya miundombinu isiyo rafiki kwenye eneo la soko hilo hususani wakati wa mvua, Nasombe ameahidi kuwa uongozi wa hamashauri hiyo utaweka moram ili kurudihsia hali nzuri sokoni hapo.