Taasisi ya Kijana Kwanza iliyopo ya Mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro , imekabidhi misaada mbalimbali ya kibinadamu kwa kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokea Aprili 24 mwaka huu wilayani humo yenye thamani ya Shilingi mil.15
Akikabidhi misaada hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi Zephaniah Sumaye, Mama Mlezi wa taasisi hiyo Apaikunda Naburi, amesema “Kijana Kwanza” ilipokea taarifa za tukio hilo kwa masikitiko makubwa mno.
“Sisi hapa tumekuja kuungana na wenzetu kwa kuwapa mkono wa pole, tumekuja na magodoro 50, mashuka, mablanketi, madaftari, kalamu, soksi, masweta, mabegi pamoja na sare za shule vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 15.”
Naburi ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mawenzi amesema Taasisi ya “Kijana Kwanza” sio mara yao ya kwanza kusaidia jamii, imekuwa ikisaidia pale ambapo jamii inapopatwa na majanga kama haya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya “Kijana Kwanza”, Sadath Sudi Ndibalemwa amesema, kutokana na janga ambalo limetokea wameona na wao kuwa sehemu ya kuwasaidia wahanga hao kwa kutoa misaada mbalimbali ya kijamii.
Taasisi ya “Kijana Kwanza” malengo yake makuu ni kuwasaidia Vijana waishio katika mazingira magumu, pamoja na jamii inayotuzunguka,”amesema Ndibalemwa.
Diwani Viti Maalum Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Elizaberth Mushi na Katibu wa CCM Kata ya Mji Mpya Clara Mlay, wameishukuru taasisi hiyo kwa namna ambavyo wameendelea kutoa msaada kwa jamii ikiwa ni kuunga mkono juhudi zaseikali za kusaidia jamii.
Awali akipokea misaada hiyo Mkuu wa Wilaya ya Moshi Zephaniah Sumaye amesema misaada hiyo aliyoipokea itakwenda kusaidia wahanga ambao walipata madhara ya mafuriko yaliyotokea Wilayani humo.
“Kipekee niwashukuru sana taasisi ya KIJANA KWANZA, wao wameonesha utofauti mkubwa sana, tumeendelea kupokea misaada mingi lakini misaada hii iliyotolewa na taasisi ya KIJANA KWANZA imekuwa na utofauti mkubwa, imelenga moja kwa moja mahitaji ambayo yapo kwa wakati huu na sisi kama serikali tunawashukuru sana.”
Aidha amewahakikishia wadau wote ambao wanaendelea kutoa misaada hiyo kupitia Kamati ya Maafa ya Wilaya wamejipanga hakutakuwa na upotevu wa missda hiyo, bali watahakikisha kila misaada inaotolewa inakwenda kuwafikia walengwa.