TPC yatoa msaada wa TZS Mil. 12 wahanga mafuriko Moshi


Kampuni ya uzalishaji sukari ya TPC Limited iliyoko Moshi, mkoani Kilimanjaro imetoa msaada wenye thamani ya shilingi mil. 12 kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokea wilaya ya Moshi, mkoani humo wiki iliyopita.

Akikabidhi msaada huo leo Aprili 30, 2024 kwa niaba ya uongozi wa kampuni hiyo, mwanasheria wa kampuni hiyo David Shilatu alisema uongozi wa TPC umeguswa na athari walizopata wananchi wa maeneo mbalimbali mkoani humo kufuatia mafuriko yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Kilimanjaro.

“Tumeguswa sana na majanga yaliyowapata wenzetu wengine wakiwa wanatoka maeneo ambayo kijiografia TPC Limited inafanya shughuli zake za kila siku”, alisema.

Alisema kuwa misaada iliyotolewa ni pamoja na magodoro 25, mablanketi 50, tani moja ya sukari, sabubi za kufulia, unga kwa ajili ya chakula, mafuta ya kupikia, maji safi na salama ya kunywa pamoja na chumvi.

Akipokea msaada huo kwa niaba ya serikali, Mkuu wa Wilaya ya Moshi Zephania Sumaye, aliushukuru uongozi wa TPC Ltd kwa misaada hiyo ambayo alisema imekuja kwa wakati muafaka.

“Uhitaji wa wenzetu waliokumbwa na janga hili kubwa ni mkubwa haswa ikitiliwa maanani zaidi ya kaya 900 zenye watu Zaidi ya 4,000 zimepoteza mali pamoja na kukosa makazi ya kuishi baada ya kuathiriwa na mafuriko makubwa yaliyotokea”, alisema.

“Ninakuweko hapa kwenye kambi hii ambayo inayowahifadhi wahanga wa mafuriko haya tangu yalipotokea; kuweko kwangu hapa kunanipa fursa ya kuona uhalisia na ukubwa wa uhitaji wa waathirika hawa kufuatia athari walizopata”, alisema na kuongeza, misaada waliyotoa TPC Ltd ni faraja kubwa kwa waathirika wa mafuriko hayo.

Aidha alisema serikali inaendelea na juhudi mbalimbali zinazolenga kurekebisha miundombinu mbalimbali iliyoharibiwa maeneo mbalimbali wilayani Moshi tangu kutokea mafuriko hayo.

“Tayari miichakato imeanza inayolenga kuhakikisha hali inarudi kuwa nzuri kwa wananchi walioathiriwa na mafuriko hayo; pia Tanroads na Tarura wameanza kuondoa vifusi vilivyoko maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo ikiwemo kwenye makazi ya watu”, alisema.




 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.