Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 Godfrey Mnzava, ameupongeza uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo agizo la Makamu wa Rais la Dk. Philp Mpango la upandaji miti kwenye maeneo ya taasisi.
Pongezi hizo zimetolewa Aprili 4, Wilayani Siha mkoani Kilimanjaro na mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kifaifa Godfrey Mnzava, baada ya Mwenge huo kuridhishwa na mradi wa ujenzi wa jengo la wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) katika hospitali hiyo.
Amesema Mwenge wa Uhuru umefurahishwa na namna ambavyo hospitali Kibong’oto inavyotekeleza Kauli Mbiu ya Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 ya “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu”.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto Dk. Leonard Subi, amesema kipindi cha miaka miwili ya 2022/2023 wamepanda jumla ya miti 3,200 ndani ya eneo la hospitali hiyo lenye heka 95.5 kwa lengo la kuendeleza juhudi za utunzaji wa mazingira ndani ya hospitali hiyo.
Katika taarifa yake ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, zilizofanyika katika Uwanja wa michezo wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu amesema mkoa huo umepanda miti takribani milioni 8 katika wilaya zote za mkoa huo.