MOSHI, KILIMANJARO
Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji nchini, wametakiwa kuongeza nguvu ya kukabiliana na changamoto zinazo kwamisha upatikanaji wa huduma za maji, ikiwemo kudhibiti tatizo la wananchi kubambikiziwa bili za maji.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso, aliyasema hayo jana wakati, akifunga kikao kazi cha Wakurugenzi wa mamlaka hizo kilichofanyika kwa siku tatu mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma bora za maji kwa wananchi.
Aweso alisema, wako baadhi ya Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji nchini wamekuwa wakiona ni fahari kwa wananchi kuendelea kukosa huduma ya maji safi na salama jambo ambalo alisema hatakubaliana nalo katika uongozi wake.
"Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji tusizoee shida za wananchi, yaani mtu kukosa maji kwako unaona ni jambo la kawaida, mwananchi ameomba kuunganishiwa maji kwa zaidi ya miezi sita na hajapata huduma hiyo, mkurugenzi upo na unaona ni jambo la kawaida, wewe hufai kuendelea kubaki katika nafasi hiyo tutakuondoa."alisema Waziri Aweso.
Alisema Wizara hiyo imeanza kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuanza matumizi ya dira za maji za malipo kabla (pre-paid meter) ili kuondokana na malalamiko ya kuwepo kwa bili bambikizi, ili kuendana na maendeleo ya kiteknolojia.
"Rais Samia Suluhu Hassan alishatoa maelekezo sisi Wizara ya Maji ni kwenda kwenye utekelezaji wa dira za maji za malipo kabla (pre-paid meter) tuanze kuzifungia taasisi za umma kisha twende kwa wananchi na tutafute mita zenye teknolojia rahisi, upatikanaji wake uwe mwepesi na gharama nafuu ili kumsaidia mwananchi kuondoa malalamiko ya kubambikiwa bili za maji,"alisema.
Awali Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Injinia Mwajuma Waziri, alitumia kikao hicho kuwahimiza Wakurugenzi hao kujenga mahusiano mema sehemu ya kazi ikiwemo kuzingatia maelekezo na maagizo ya viongozi katika utendaji kazi wa majukumu yao.
"Wizara ya Maji bila kuwa na mshikamano, bila kuwa na upendo, hatuwezi kufanya kazi kwa uadilifu kama ambavyo tunaelekezwa na viongozi wetu ngazi za juu hivyo twendeni tukadumishe upendo na mshikamano lakini pia kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa kuwasikiliza wananchi pamoja na kutatua kero zao kwa wakati."alisema Injinia Waziri.
Naye Mwenyekiti wa Wakurugenzi watendaji Mamlaka za Maji Tanzania Bara Injinia Patrick Nzamba alisisitiza Wizara hiyo kuja na mpango wa Kitaifa wa ununuzi na ufungaji wa dira za maji za malipo kabla (Pre-Paid Meter) kwa mamlaka hizo.