KIBONG'OTO, SANYA JUU-SIHA
Fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 zilizoanzishwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, zimendelea kuzaa matunda mazuri, ambapo zimewezesha kujenga mradi wa jengo la wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) katika hospitali ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto, iliyopo Wilaya ya Siha mkoa wa Kilimanjaro lililogharimu Sh bilioni 1.3.
Mkurugenzi wa hospitali hiyo Dk Leonard Subi, aliyasema hayo wakatia alipokuwa akiwasilisha taarifa ya uanzishwaji wa mradi wa ukarabati wa jengo la wagonjwa mahututi (ICU) kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 Godfrey Mnzava na timu yake wakati wa uzinduzi wa jengo hilo.
“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa mradi huu wa kihistoria, ni wa kihistoria kwa maana kwamba, tangu hospitali hii ianzishwe miaka 98 iliyopita, haijawahi kuwa na chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), kitengo ambacho ni muhimu sana linapokuja suala la kutoa matibabu hasa. kwa kuzingatia ukweli kwamba, matibabu tunayotoa hapa ni mahususi kwa magonjwa ya kuambukiza kikiwemo Kifua Kikuu (TB)”, alibainisha.
Aliendelea kusema kuwa, mradi huo uliohusisha ukarabati wa jengo moja la zamani ambalo lilibadilishwa kuwa ICU, ulitekelezwa kwa kuzingatia miongozo yote ya Serikali wakati wa utekelezaji wake.
Dk. Subi aliendelea kusema kuwa, pamoja na ukarabati huo, mradi huo pia ulihusisha kuweka mfumo wa umeme, mfumo wa tiba ya oksijeni, mfumo wa IT, mfumo wa maji safi na ukarabati wa mazingira ya nje ya hospitali hiyo.
"Vifaa vilivyonunuliwa kwa ajili ya kitengo hicho kipya ni pamoja na vitanda 10 maalum kwa ajili ya wagonjwa wa ICU, mashine 10 za kupumulia, mashine 10 za kufuatilia wagonjwa, Defibrillator moja, vifaa vya Ultrasound, Suction Machine pamoja na vifaa vingine vya matibabu vinavyohitajika katika chumba cha wagonjwa mahututi”, alisema.
Aidha, alisema hospitali hiyo imepokea vitanda na vifaa vingine vya matibabu kutoka Bohari ya Dawa (MSD) kwa kitengo cha ICU, ambapo alisema (ICU) hiyo ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 20 mahututi kwa wakati mmoja.
Aliongeza kusema kuwa jumla ya wataalam 16 wa hospitali hiyo, walipatiwa mafunzo maalum ya matumizi ya vifaa tiba vinavyohusiana na huduma zinazotolewa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na kwamba wataalam hao ni pamoja na madaktari sita, wauguzi wanane na wataalam wawili wa TEHAMA ambao alisema walipatiwa mafunzo maalum katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando iliyopo Mwanza na katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam”, alisema.
Akizungumzia uhusiano wa kituo hicho cha afya na mbio za Mwenge wa Uhuru 2024, Dk Subi alisema uongozi wa hospitali hiyo umetekeleza kwa vitendo moja ya Kauli Mbiu ya mbio za mwaka huu inayohusiana na mazingira kwa kupanda miti 3,200 ndani ya eneo la hospitali hiyo ambayo alisema ilikuwa na eneo la ekari 95.5.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuzindua mradi wa ICU, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 Godfrey Mnzava, aliwataka wasimamizi wa hospitali hiyo kuhakikisha miundombinu na mali nyingine za hospitali hiyo zinatunzwa ili zidumu kwa muda mrefu kuhudumia watu.
“Rais Dk Samia Suluhu Hassan na Serikali yake yote wanafanya kazi usiku na mchana kuboresha hali ya wananchi nchini na hiyo ni pamoja na sekta ya afya ambayo Rais amekuwa bingwa; moja ya njia ya kumuunga mkono yeye na serikali katika mipango yake ni kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa nchini inalindwa”, alisema.