MOSHI,CCM-MKOA KILIMANJARO
Balozi
wa Msumbiji nchini Tanzania Rocardo Amrosio Mtumbuida amewataka raia wa
taifa hilo wanaoishi nchini Tanzania kujiandaa kupiga kura katika
uchaguzi mkuu wa taifa hilo utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Akizungumza
mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro kaskazini mwa Tanzania waati wa ziara
yake ya siku moja Balozi huyo aliuambia mkutano wa viongozi wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) chenye mafungamano na chama cha FRELIMO nchini Msumbiji
kuwa raia wa Msumbiji wanaoishi nje ya taifa lao kuwa mwaka huu ni
mwaka wa uchaguzi.
“Watu
wa Msumbiji mwaka huu tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge
na Wakuu wa Mikoa, Tayari uchaguzi wa Serikali za Mitaa ulishafanyika
mwaka jana, sasa tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu,” alisema
Balozi Mtumbuida.
““Nimekuja
kuwaomba viongozi wangu wa CCM mtusaidie kuwahamasisha raia wetu wa
Msumbiji wanaoishi Kilimanjaro, itakapofika Oktoba mwaka huu wajitokeze
kwa wingi kwanda kukipiga kura chama cha Frelimo ili kiweze kuendelea
kuwa imara,” alisisitiza.
Balozi
Mtumbuida amesema miaka mitano iliyopita kumefanyika mabadiliko mengi
katika katiba yao likiwamo suala la uchaguzi wa wakuu wa mikoa ambalo
hapo awali halikuwepo ambapo mwaka huu watafanya uchaguzi wa viongozi
hao
“Bunge wa Msumbiji lina viti 250 na chama cha Flelimo kinaongoza kwa asilimia 94 ya Wabunge wote, na uchaguzi wa mwaka huu tunatamani kufikia asilimia 100. Kipindi cha miaka mitano iliyopita zoezi la kuwachagua Wakuu wa Mikoa halikuwepo , lakini baada ya mabadiliko ya Katiba kwa mara ya kwanza tunakwenda kufanya uchaguzi wa Wakuu wa Mikoa,” aliongeza Balozi Mtumbuida.
Oktoba
9, 2024 Msumbiji itafanya uchaguzi mkuu, ambapo Diaspora wa Msumbiji
waliopo nchini Tanzania hususani mkoani Kilimanjaro watakuwa na kituo
cha wapiga kura siku hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini Faraji Kibaya Swai; alisema ziara
ya Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania imemkumbusha mambo mengi sana,
wakati ule wa harakati za kutafuta ukombozi Kusini mwa Afrika, Tanzania
ilikuwa mstari wa mbele chini ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, ambaye aliweza kuweka undugu baina yetu na Msumbiji.
“Nakumbuka nikiwa Chuoni , tulikuwa tunatoa damu kwa ajili ya wapigania Uhuru kule nchini Msumbiji , undugu wetu na nchi ya Msumbiji ni damu.Ninamshukuru sana Balozi ameonesha kuendeleza undugu wetu kwa kuja katika mkoa wetu wa Kilimanjaro hususan hapa Moshi mjini na kuzungumza na Wanachama wa CCM,” alisema Swai.