Jumuiya ya Wazazi CCM Kilimanjaro yatoa ufafanuzi kuhusu mgogoro wa mipaka ya Kibo Shanty Primary Academy



SHANTY TOWN, KATA YA KILIMANJARO

Uongozi wa shule ya msingi ya Kibo-Shanty Primary Academy, wameulalamikia uongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, kuja na kuziba eneo ambalo walikuwa wakilitumia kwa ajili ya magari ya shule hiyo, kupakia na kushusha wanafunzi na kuchimba mtaro jambo ambalo limeleta usumbufu kwa wanafunzi hao kuweza kuingia madarasani.

Akiongea na waandishi wa habari kuhusiana na lalamiko hilo mmoja wa Wakurugenzi wa shule hiyo Ibrahimu Shayo (Ibra Line) amesema ya kuwa eneo hilo limeingiliwa na Jumuiya ya Wazazi kwa kufanya ujenzi katika eneo hilo.

Shayo amesema kuwa eneo hilo limechimbwa mtaro na kuzuia magari ya shule ya wanafunzi kukosa maeneo ya kupakia na kushushia wanafunzi.

“Taarifa tuliyo nayo ni kuwa eneo hilo kuna ujenzi wa bwalo la wanafunzi wa shule ya sekondari ya Kibo, ambayo tuko nayo jirani; pamoja na kupewa taarifa kuhusiana na ujenzi huo lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu tulikuwa hatukuwa tayari kupisha shughuli hiyo kwa sababu ambayo tulishawajulisha uongozi Jumuiya ya Wazazi ambayo inamiliki sekondari hiyo”, amesema Shayo.

Ameongeza kuwa “Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Kilimanjaro ilituandikia barua ili tuache kutumia eneo hilo na badala yake tujenge geti la shule yetu, lakini na sisi tuliwajibu kwa barua ya kuwa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa sasa greda ambalo tungelitumia kwa ajili ya shughuli za kutengeneza geti letu haliwezi kuingia pale kwa vile litatitia”, amesema Shayo.

Hata hivyo, Ibrahimu Shayo (Ibra Line) amesema pamoja na kutoa majibu ya barua yao bado tumeshuhudia eneo hilo likichimbwa msingi kwa ajili ya ujenzi wa bwalo hali ambayo imeleta  changamoto ya wanafunzi kushindwa kuingia madarasani kutokana na eneo hilo kuchimbwa mtaro mkubwa.

Akizungumzia swala hilo Mwenyekiti wa Wazazi Mkoa wa Kilimanjaro Daudi Babu Mrindoko, amesema uongozi wa Jumuiya hiyo, uliwapa maelekezo na muda wa shule hiyo kutengeneza geti lao wakati wa mapumziko mafupi ya Pasaka lakini bado hatujaona wakitoa ushirikiano wowote.

“Tuna mradi wetu wa ujenzi wa bwalo la shule ya sekondari Kibo, tumeanza ujenzi  huo hivi karibuni katika eneo hilo ambalo linalalamikiwa mmoja wa watu ambae anajiita ni miongoni mwa Wakurugenzi katika shule hiyo ya msingi japo kuwa sisi hatumtambui,”.

Mrindoko amesema hii ni sehemu ya mipango ya Jumuiya ya Wazazi ya kujenga bwalo  ambalo linahitajika sana katika shule ya sekondari ya Kibo kwa muda mrefu kiasi cha wanafunzi kulazimika kula chakula chini ya miti”, amesema.

Aidha amesema tayari mipaka kati ya shule hizo mbili ilishaainishwa tangu kuanzishwa kwa shule hiyo ya msingi, ilikuepuka sababu mbalimbali ikiwemo ile ya wanafunzi wa shule ya sekondari kuchangamana na wale wa shule ya awali na msingi.

Mrindoko amesema hakuna haja ya wazazi kuwa na wasiwasi wowote kuhusiana na swala hilo kutokana na kuwa ujenzi unaoendelea ni maendeleo ya shule ya sekondari Kibo na kwamba uongozi wa shule ya msingi tayari walishataarifiwa kuhusiana na swala hilo.

“Pamoja na hoja yao ya mvua kuzuia shughuli za kujenga geti lao kama inavyohitajika, uongozi wa shule hiyo ya msingi wamelima mahindi, sasa hapa tujiulize lamawa dhidi ya Jumuiya inatoka wapi”, ameongeza kusema Mrindoko.

Kwa upande wake Katibu wa Wazazi  Wilaya ya Moshi Mjini Nada Orry, amesema Jumuiya ya Wazazi ilitenga ekari 4.5 kwa ajili ya shule hiyo ya msingi, hivyo ni vyema kila shule ikaheshimu mipaka yake.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro Chifu Daudi Mrindoko akielekeza jambo katika viunga vya Shule ya Kibo Shanty mnamo Aprili 8, 2024 baada ya fununu za kutokea kwa vurugu shuleni hapo.


Mwonekano wa Shule ya Msingi Kibo Shanty Primary Academy 


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.