SIHA-KILIMANJARO.
WATANZANIA wanaotumia dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI (ARV) wametakiwa kuzingatia maelekezo wanayopewa na wataalamu wa afya, ikiwemo kutokukatisha dozi au kuacha kutumia dawa bila ushauri wa kitaalamu, kwa kuwa kufanya hivyo kunaweza kuchangia virusi kujenga usugu dhidi ya dawa na kupunguza ufanisi wa matibabu.
Meneja wa Maabara ya Afya ya Jamii Ngazi ya Tatu ya Usalama kutoka Taasisi ya Magonjwa ya Kuambukiza Tanzania (TIDI), Dk. Shaban Mziray,aliyasema hayo Agosti 3,2026, wakati akitoa maelezo kwa wazee maarufu, viongozi wa dini, viongozi wa Serikali pamoja na viongozi wa kimila na jadi waliotembelea taasisi hiyo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
Amesema kuwa matumizi yasiyo sahihi ya ARV, ikiwemo kuruka dozi mara kwa mara au kuacha dawa bila maelekezo ya mtaalamu, yanaweza kuongeza uwezekano wa virusi kubadilika na kuwa sugu dhidi ya baadhi ya dawa zinazotumika katika matibabu.
Amesema kuwa baadhi ya watu wanaoishi na VVU hushindwa kuendelea vizuri na matibabu kutokana na kutofuata maelekezo ya wataalamu wa afya, ikiwemo kukatisha dozi, kusahau au kuacha kutumia dawa kwa muda uliopangwa.
Amesema matumizi yasiyo sahihi ya dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI (ARV) yanaweza kuchangia VVU kujenga usugu dhidi ya dawa hizo, hali inayoweza kufanya matibabu kutokuwa na ufanisi.
Amesema kuwa miongoni mwa sababu zinazoweza kuchangia usugu wa vimelea dhidi ya dawa ni kukatisha dozi, kuacha kutumia dawa kabla ya muda uliopangwa mara baada ya mtu kujisikia vizuri, pamoja na matumizi holela ya dawa bila ushauri wa wataalamu wa afya.
Aidha Dk. Mziray ameonya matumizi holela ya dawa nyingine, ikiwemo antibiotiki, bila ushauri wa mtaalamu wa afya, hali hiyo inaweza kuchangia kuongezeka kwa usugu wa vimelea dhidi ya dawa
Amesema changamoto ya usugu wa dawa si kwa VVU pekee, bali ni tatizo linaloendelea kuonekana pia kwa vimelea vinavyosababisha magonjwa mbalimbali ambayo hutibiwa kwa dawa.
Kwa mujibu wa Dk. Mziray, amesema maabara ya TIDI inafanya ufuatiliaji wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa zinazotumika katika matibabu ya magonjwa mbalimbali, pamoja na uchunguzi wa utendaji kazi wa viungo kama ini na figo, homoni na vimelea vya magonjwa kwa kutumia njia mbalimbali, ikiwemo za kimolekuli.
Aidha, amesema maabara hiyo hufanya tathmini ya kiwango cha dawa mwilini, hatua inayosaidia wataalamu kuboresha matibabu na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma kulingana na mahitaji yao.
Amesema uwepo wa Maabara ya Usalama wa Kibiolojia Daraja la Tatu (BSL-3) katika taasisi hiyo ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa nchi wa kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza na kudhibiti usambazaji wa vimelea hatarishi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa TIDI, Dk. Leonard Subi, amesema magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwemo magonjwa ya figo, moyo na saratani, yanaendelea kuongezeka duniani, hususan barani Afrika.
Amesema hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya mtindo wa maisha, ikiwemo unywaji wa pombe kupita kiasi, uvutaji wa sigara, matumizi ya tumbaku, kutofanya mazoezi na matumizi yasiyo sahihi ya dawa.
Dk. Subi aliwataka Watanzania kuzingatia mtindo bora wa maisha, kufanya mazoezi na kuepuka matumizi holela ya dawa ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kwa afya.
![]() |










