DIWANI WA KIUSA KUFANYA ZIARA YA MGUU KWA MGUU KUSIKILIZA KERO ZA WANANCHI

KIUSA-MOSHI

DIWANI wa Kata ya Kiusa katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Khalid Shekoloa, anatarajia kufanya ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya kata hiyo kwa kutembea kwa miguu, kwa lengo la kusikiliza na kufahamu kero zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.

Shekoloa ameyasema hayo mjini Moshi Oktoba 22,2026 wakati akizungumza na KISENA UPDATE BLOGSPOT, kuhusiana na ziara hiyo, ambapo amesema ziara hiyo itamwezesha kukutana ana kwa ana na wananchi, kusikiliza changamoto zinazowakabili na kupata maoni yao kuhusu masuala mbalimbali yanayohitaji kufanyiwa kazi ili kuboresha huduma na maendeleo katika kata hiyo.

Amesema kupitia ziara hiyo, atapata fursa ya kufahamu kwa undani changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo wanayoishi, hatua itakayosaidia kutambua vipaumbele na kutafuta namna ya kushughulikia kero hizo kwa kushirikiana na mamlaka husika.

Aidha, amesema katika ziara hiyo atatoa elimu kwa wananchi kuhusu mvua za El Nino na tahadhari wanazopaswa kuchukua ili kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza, yakiwemo mafuriko na athari nyingine zinazoweza kuhatarisha usalama wa watu na mali zao.

Amesisitiza umuhimu wa wananchi kuzingatia maelekezo ya wataalamu na kuchukua hatua za tahadhari mapema, huku akieleza kuwa ziara hiyo inalenga kuimarisha mawasiliano kati ya wananchi na uongozi wa kata ili changamoto zinazowakabili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.