MOSHI-KILIMANJARO.
WANANCHI wanaoishi karibu na mito wametakiwa kuheshimu maeneo ya hifadhi ya mito kwa kuepuka kufanya shughuli za kilimo ndani ya mita 60 zilizotengwa, ili kulinda vyanzo vya maji na kupunguza athari za mafuriko yanayosababishwa na kuharibika kwa mikondo ya mito.
Wito huo umetolewa jana na Mhandisi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB), Omary Gumbo, wakati akizungumzia kazi ya kudabua tope na mchanga katika Mto Ghona, uliopo katika Kijiji cha Ghona, Kata ya Kahe Mashariki, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na mvua za El Niño.
Gumbo alisema shughuli za kibinadamu zinazofanyika ndani ya hifadhi za mito, ikiwemo kilimo, huchangia mmomonyoko wa udongo na kusababisha tope na mchanga kujaa kwenye mito, hali inayopunguza uwezo wake wa kupitisha maji na kuongeza hatari ya mafuriko.
Alisema Bodi ya Maji Bonde la Pangani imeshirikiana na mdau Sabasi Woisso katika kazi ya kuondoa tope na mchanga uliokuwa umejaa katika Mto Ghona na kuufanya kupoteza mwelekeo wake, hali iliyokuwa ikisababisha maji kujaa na kuingia katika makazi ya wananchi.
Kwa mujibu wake Mhandisi Gumbo, alisema mdau huyo alisaidia upatikanaji wa mtambo wa kudabua tope, huku bonde likitoa utaalamu na mafuta kwa ajili ya kuendesha mtambo huo.
Alifafanua kuwa hadi wakati huo, kazi ya kudabua ilikuwa imefikia umbali wa kilomita 3.7, hatua inayolenga kurejesha uwezo wa mto kubeba maji mengi na kupunguza uwezekano wa maji kutoka nje ya mkondo wake wakati wa mvua kubwa.
Alisema awali, kujaa kwa tope na mchanga kulisababisha maji kuelekea kwenye makazi ya watu na kuleta uharibifu wa mali na shughuli za kiuchumi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ghona, Shwahibu Mrisha, alisema wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakikabiliwa na mafuriko makubwa kila mwaka, yaliyokuwa yakiharibu mashamba na makazi pamoja na kusababisha mifugo kusombwa na maji.
Alisema hali hiyo ilichangiwa na mto huo kujaa tope, mchanga na magogo yaliyokuwa yakiletwa na maji wakati wa mvua.
Mrisha alisema kijiji hicho kina wakazi takribani 250, ambapo kati yao 175 walikuwa wakiathiriwa na mafuriko kabla ya kazi ya kudabua mto kuanza na kwamba athari hizo zilikuwa zikifika pia katika Kijiji cha Kyomu.
Alisema wana matumaini kuwa kuondolewa kwa tope na kuongezwa kwa kina cha mto kutasaidia kupunguza athari za mafuriko katika msimu wa mvua unaotarajiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kyomu, Kata ya Kahe Mashariki, Josamu Kundael, alisema maeneo ya Kitongoji cha Paplic na Majengo yalikuwa miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko, yaliyokuwa yakiharibu mashamba, makazi na mifugo ya wananchi.
Alisema hatua za kurekebisha mkondo wa Mto Ghona ni muhimu kwa usalama wa wakazi wa vijiji hivyo.
Mkazi wa Kijiji cha Ghona B, Joyce Mchome, alisema nyumba nyingi katika eneo hilo zimejengwa kwa miti na udongo, hivyo kuwa katika hatari ya kuharibika wakati wa mafuriko.
Alisema maji yalipovamia makazi yao, baadhi ya nyumba zilianguka au kudidimia, huku mali na mifugo vikisombwa na maji.
Naye mkazi mwingine wa Kijiji cha Ghona, Ibrahim Ndakama, alisema Mto Ghona ulianza kupoteza mwelekeo wake tangu miaka ya 1980 kutokana na maji yaliyokuwa yakibeba udongo na magogo, yaliyosababisha kina cha mto kujaa.
Alisema wakati mwingine wakazi walilazimika kuondoka majumbani mwao pamoja na mifugo usiku wa manane ili kujinusuru na mafuriko.
Akizungumza Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumiaji wa Maji ya Mto Ghona, Bakari Mmbaga, alisema shughuli za kilimo zinazofanyika kando ya mto zimechangia mmomonyoko wa udongo na kuongezeka kwa mchanga ndani ya mto.
Alisema licha ya Bodi ya Maji Bonde la Pangani kutoa elimu kuhusu uhifadhi wa vyanzo vya maji, baadhi ya wananchi wameendelea kufanya shughuli zinazoharibu maeneo hayo, hali inayochangia maji kuacha mikondo yake na kuelekea kwenye makazi ya watu.

















