KIUSA-MOSHI
DIWANI wa Kata ya Kiusa, katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Khalid Shekoloa, ameahidi kutoa zawadi ya Shilingi 50,000 kwa kila mwanafunzi atakayepata daraja la kwanza (Division One) na Shilingi 30,000 kwa atakayepata daraja la pili (Division Two) katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha ufaulu bora katika Shule ya Sekondari Kiusa.
Aidha, amesema ataweka motisha ya fedha kwa walimu watakaofanya vizuri katika kuwaandaa wanafunzi na kuboresha matokeo ya shule hiyo.
Shekoloa alitoa ahadi hiyo leo Ijumaa, Oktoba 16, 2026, alipotembelea shule hiyo na kuzungumza na watahiniwa 180 wanaotarajia kufanya mtihani huo, akiwa ameambatana na Mtendaji wa Kata ya Kiusa, Davita Tesha.
Diwani huyo aliwataka wanafunzi kuongeza bidii katika marudio ya masomo, kuzingatia maelekezo ya walimu na kutumia vizuri muda uliobaki ili waweze kupata matokeo yatakayowawezesha kuendelea na elimu ya juu.
“Wanafunzi wa kidato cha nne watakaopata daraja la kwanza na la pili nitawapatia zawadi yangu mwenyewe, mkifaulu wote kwa kupata daraja la kwanza, kila mmoja nitampa Shilingi 50,000, na wale watakaopata daraja la pili kila mmoja nitampa Shilingi 30,000,” alisema Shekoloa.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kata ya Kiusa, Davita Tesha, aliwahimiza watahiniwa hao kuwa na nidhamu, kujiamini na kuzingatia ratiba zao za maandalizi ya mitihani.
Aliwataka kuepuka mambo yanayoweza kuwavurugia masomo na kutumia maarifa waliyopata kutoka kwa walimu wao ili kufanya vizuri, akisisitiza kuwa matokeo bora yanahitaji juhudi, kujituma na ushirikiano kati ya wanafunzi, walimu na wazazi.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kiusa, Mariagoreth Maliga, alisema shule hiyo imeonesha maendeleo katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne.
Alieleza kuwa mwaka 2024 wanafunzi watatu walipata daraja la kwanza, 12 daraja la pili na 25 daraja la tatu, huku kiwango cha ufaulu kikiwa asilimia 28.7.
Alisema Mwaka 2025, wanafunzi saba walipata daraja la kwanza, 32 daraja la pili na 38 daraja la tatu, huku kiwango cha ufaulu kikiongezeka hadi asilimia 57.
Kwa mwaka huu wa 2026, shule hiyo ina watahiniwa 180 wanaotarajia kufanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne (CSEE), unaotarajiwa kuanza Oktoba 19 na kukamilika Novemba 6.
"Motisha iliyotangazwa na diwani huyo inalenga kuongeza hamasa kwa watahiniwa kufanya vizuri, huku matarajio yakiwa ni kuendeleza mwenendo wa kuimarika kwa matokeo ya shule hiyo."alisema Mwl. Maliga.
Akizungumza kwa niaba ya wazazi, Hamisi Mkenda alimshukuru Shekoloa kwa kuahidi kutoa zawadi kwa wanafunzi watakaofanya vizuri, akisema hatua hiyo inaweza kuwapa wanafunzi hamasa ya kuongeza juhudi katika masomo na kuwasaidia wazazi kugharamia baadhi ya mahitaji ya elimu watoto wanapoendelea na ngazi za juu za masomo.






