SAME, KILIMANJARO.
HIFADHI ya Taifa ya Mkomazi imeendelea kufungua fursa kwa wawekezaji wanaotaka kujenga hoteli za kitalii ndani ya hifadhi hiyo, hatua inayolenga kuongeza huduma za malazi na chakula kwa watalii wanaotembelea eneo hilo.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Eva Mallya, alisema hayo wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari waliotembelea hifadhi hiyo katika ziara maalumu ya kuitangaza na kuhamasisha utalii wa ndani.
Mallya alisema hifadhi hiyo ina maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji wa huduma za malazi, hivyo kuwapa fursa wawekezaji kujenga hoteli zitakazowawezesha watalii kupata mahali pa kulala wanapotembelea vivutio mbalimbali vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo.
Alisema sambamba na kufungua fursa kwa wawekezaji, hifadhi hiyo inaendelea kuboresha huduma za malazi kwa watalii wa ndani, ikiwemo kuongeza uwezo wa nyumba za kulala wageni aina ya kotage, ambazo kwa sasa zina vitanda 18, ili kuweza kuhudumia wageni wengi zaidi.
Aliongeza kuwa kuna mpango wa kujenga hosteli zitakazotumika kuwahudumia wanafunzi wa shule na vyuo watakaotembelea hifadhi hiyo kwa shughuli za utalii na mafunzo, hatua itakayoongeza uwezo wa hifadhi kupokea makundi makubwa ya wageni.
Akizungumzia miundombinu ya barabara, Mallya alisema takribani asilimia 75 ya barabara za hifadhi hiyo zinapitika mwaka mzima, huku maeneo machache yakihitaji kuboreshwa ili kuhakikisha watalii wanaweza kufika katika sehemu mbalimbali za hifadhi bila kuathiriwa na hali ya barabara.
Alisema lengo ni kuendelea kuboresha miundombinu hiyo kadiri fedha zinavyopatikana, ili barabara zote ziweze kupitika mwaka mzima na kurahisisha usafiri wa watalii ndani ya hifadhi hiyo.
Aidha, alisema hifadhi hiyo inaendelea kuimarisha muunganiko wa barabara upande wa mashariki na magharibi, ikiwemo njia zinazounganisha Tanga kupitia lango la Umba na Lushoto kupitia lango la Kamakota, ili maeneo hayo yaweze kufikika kwa urahisi kipindi chote cha mwaka.
Mallya aliwahimiza Watanzania kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ili kujionea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo, wakiwemo Faru Weusi, Twiga, Nyati, Chui, Tembo, Simba na Swala Twiga










