MAMBA-MYAMBA.
SERIKALI mkoa wa Mkoa wa Kilimanjaro, imeitaka Halmashauri ya Wilaya ya Same kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vidogo vya kuongeza thamani ya mazao na viungo ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi, kuongeza kipato cha wakulima wadogo na kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa mkoa huo Nurdin Babu, wakati wa hafla ya kuhitimisha mradi wa Mkondo wa Maji wa Saseni, iliyofanyika katika Kata ya Mamba Myamba, wilayani Same, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuweka mikakati itakayowawezesha wakulima kunufaika zaidi na mazao wanayozalisha.
Katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Hassan Bomboko, kwa niaba yake, Babu alisema uanzishwaji wa viwanda vidogo vya kuchakata mazao utawasaidia wakulima kuuza bidhaa zilizoongezwa thamani badala ya kutegemea soko la mazao ghafi, hatua itakayowawezesha kupata faida kubwa na kuongeza fursa za ajira na biashara kwa wananchi.
Aidha, aliwapongeza viongozi wa Floresta Tanzania kwa kubuni na kutekeleza mradi huo, akisema umekuwa na mchango katika kuboresha uzalishaji wa kilimo, usalama wa chakula na kipato cha wakulima.
Alieleza kuwa asilimia 80 ya wakulima wamenufaika na mavuno bora kupitia elimu ya kilimo inayotolewa na taasisi hiyo, huku juhudi za kuboresha upatikanaji wa mbegu bora na mnyororo wa thamani wa mboga na viungo zikichangia maendeleo ya sekta ya kilimo mkoani Kilimanjaro.
Pia amewataka wananchi, taasisi mbalimbali, hoteli na waendeshaji wa shughuli za utalii kujenga utamaduni wa kununua bidhaa zinazozalishwa nchini ili kupanua soko la wakulima na wajasiriamali, kuongeza uzalishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Aidha, amewataka viongozi na wananchi wa Same kushirikiana kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana kupitia mradi huo yanaendelezwa hata baada ya kukamilika kwa shughuli zake.
Akiwasilisha taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi wa Floresta Tanzania, Richard Mhina, alisema shughuli zake zilianza mwaka 2010 katika maeneo ya Mpinji, Myamba, Bwambo, Lugulu, Kirangare, Mtii na Vunta.
Alisema katika kipindi cha utekelezaji, vikundi 138 vya huduma ndogo za kifedha vilianzishwa, huku wanachama wake wakiweka akiba ya Shilingi milioni 980 na kuwezesha kutolewa kwa mikopo yenye thamani ya Shilingi milioni 710 kwa ajili ya kuanzisha na kupanua shughuli mbalimbali za uzalishaji.
Mhina aliongeza kuwa mradi huo umechangia pia kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu upandaji miti na uhifadhi wa mazingira, ambapo jumla ya miti miioooni 2.5 imepandwa katika eneo la Mkondo wa Maji wa Saseni, huku wanafunzi 102,000 wakipatiwa elimu ya uhifadhi wa mazingira katika kipindi cha utekelezaji wa mradi huo.












