SIHA-KILIMANJARO.
TAASISI ya Magonjwa ya Kuambukiza Tanzania (TIDI), imeandaa mdahalo utakaowakutanisha wazee maarufu, viongozi wa dini, pamoja na viongozi wa mila na jadi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
Mdahalo huo unatarajiwa kufanyika Septemba 3 mwaka huu katika ukumbi wa TIDI, ambapo washiriki watapata fursa ya kujadili historia ya taasisi hiyo, maendeleo yake pamoja na mwelekeo wake kuelekea miaka 100 ya huduma kwa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Septemba 2 mwaka huu, Kaimu Mkurugenzi wa TIDI, Dk. Leonard Subi, alisema wameamua kuwashirikisha wazee na viongozi hao kwa kuwa wana nafasi muhimu katika kuhifadhi historia na kutoa ushauri kuhusu maendeleo ya taasisi hiyo.
Alisema wazee hao wanaifahamu kwa undani historia ya TIDI, ambayo hapo awali ilijulikana kama Hospitali Maalumu ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong’oto (KIDH), hivyo ushiriki wao ni muhimu katika maadhimisho hayo.
Dk. Subi alisema kupitia mdahalo huo, wazee na viongozi hao watapata fursa ya kuona hatua iliyofikiwa na taasisi hiyo, ikiwemo uwekezaji mkubwa uliofanyika katika miundombinu, vifaa na teknolojia za kisasa za utoaji wa huduma za afya.
“Tunapoenda kuadhimisha miaka 100, ni vizuri wazee hawa wakashiriki katika maadhimisho haya, kwa sababu wanaifahamu zaidi historia ya Taasisi ya Magonjwa ya Kuambukiza Tanzania, tumeona ni muhimu kuwashirikisha ili tupate maono na ushauri wao,” alisema Dk. Subi.
Alisema washiriki pia wataelezwa mwelekeo wa taasisi hiyo na namna ilivyojipanga kutoa huduma bora zaidi, huku wakipata fursa ya kutoa mawazo na michango yao katika safari ya TIDI kuelekea miaka mingine ya huduma kwa wananchi.
Dk. Subi alisema taasisi hiyo haiwezi kuadhimisha miaka 100 bila kuwashirikisha watu wenye historia na uelewa wa eneo hilo, kwa kuwa shughuli hiyo inafanyika katika jamii ambayo imekuwa sehemu ya historia ya Kibong’oto.
Aidha, alisema mdahalo huo utakuwa fursa kwa TIDI kuwaelimisha wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi hiyo, ikiwemo huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika magonjwa ya kuambukiza.
"Pamoja na huduma za tiba, TIDI inajihusisha pia na tafiti, mafunzo na utafiti katika maeneo mbalimbali yanayohusiana na magonjwa ya kuambukiza."alisema.
Dk. Subi alisema mdahalo huo pia utatumika kutoa taarifa kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya miaka 100 na kuwaeleza washiriki namna taasisi ilivyojipanga kuelekea kilele cha maadhimisho hayo.
Alisema kilele cha maadhimisho ya miaka 100 ya Hospitali ya Kibong’oto, ambayo sasa ni TIDI, kinatarajiwa kufanyika Novemba 26 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Dk. Subi, kupitia mdahalo huo viongozi hao watapata nafasi ya kushiriki katika mjadala wa historia, mafanikio na mwelekeo wa taasisi hiyo, huku wakitumia jukwaa hilo kuwafikishia wananchi taarifa kuhusu huduma zinazotolewa na TIDI.
Alisema ushirikishwaji wa jamii katika maadhimisho hayo ni muhimu katika kuendeleza uhusiano kati ya taasisi hiyo na wananchi, pamoja na kuhakikisha historia ya miaka 100 ya TIDI inaendelea kuhifadhiwa na kueleweka kwa vizazi vijavyo.







