TIMAD FC YAFANIKIWA KUTWAA UBINGWA KOMBE LA WILAYA

MOSHI-KILIMANJARO.

TIMAD FC imeibuka mabingwa wa Kombe la ubingwa Wilaya ya Moshi msimu huu, baada ya kuonesha kiwango kizuri katika mashindano hayo yaliyolenga kutoa nafasi kwa vijana wanaochipukia katika mchezo wa soka kuonesha vipaji vyao.

Akizungumza baada ya kutwaa ubingwa huo, Mkurugenzi wa Kituo cha TIMAD na Mwalimu Mkuu wa timu hiyo, Mohamed Msemo, amesema mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za timu hiyo katika kuwaendeleza vijana, huku akieleza kuwa TIMAD FC ilikuwa miongoni mwa timu zilizoshirikisha wachezaji wadogo zaidi.

Msemo amesema anajivunia timu yake kwa kutwaa ubingwa huo licha ya kuwa na wachezaji wenye umri mdogo ukilinganisha na timu nyingine zilizoshiriki mashindano hayo.

Amesema mashindano hayo yamekuwa fursa muhimu kwa vijana kuonesha vipaji vyao, huku akiviomba vituo na taasisi mbalimbali vinavyohusika na malezi na makuzi ya watoto kuendelea kuwapa nafasi vijana kushiriki katika michezo.

“Naishukuru timu yangu kwa kuibuka mabingwa na kuchukua Kombe la Wilaya msimu huu, kati ya timu zote zilizoshiriki, timu yangu ndiyo iliyokuwa na watoto wadogo sana, lakini imeweza kuibuka na ushindi,” amesema Msemo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijana Kwanza FC, Mujibu Abeid, amezipongeza TFF na KRFA kwa kuunga mkono mashindano yaliyowapa vijana nafasi ya kuonesha uwezo wao katika soka.

Amesema mashindano hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kubaini vipaji vipya, akieleza kuwa mchezo wa kirafiki kati ya TIMAD FC na Kijana Kwanza FC uliochezwa baada ya kumalizika kwa mashindano hayo ulikuwa sehemu ya shughuli za kuhitimisha mashindano na kukabidhi kombe kwa mabingwa.

Mujibu amesema Kijana Kwanza FC imeamua kuwekeza zaidi katika soka la vijana kwa kuwapa nafasi wachezaji wa rika mbalimbali, wakiwemo wenye umri wa miaka 15, 17 hadi 20, ili kuwaandaa kwa ushindani mkubwa zaidi siku zijazo.

Naye Katibu wa Chama cha Mpira wa miguu Wilaya ya Moshi, Japhet Mpande, ameipongeza TIMAD FC kwa kutwaa ubingwa wa Wilaya msimu huu, huku akiishukuru Kijana Kwanza FC kwa kukubali kushiriki mchezo wa kirafiki uliolenga kuhitimisha shughuli za mashindano hayo.

Mpande amesema baada ya TIMAD FC kutwaa ubingwa, waliamua kuitafuta timu nyingine ili kucheza mchezo wa kirafiki kabla ya kukabidhi rasmi kombe hilo, hatua iliyolenga kufanya hafla hiyo iwe na mvuto zaidi kwa wachezaji na mashabiki.

“TIMAD tayari walikuwa wameshinda, tukaona si vizuri kuwakabidhi kombe lao bila ya shughuli nyingine, tulialika Kijana Kwanza FC kucheza mchezo wa kirafiki na baadaye tukawakabidhi kombe lao,” amesema Mpande.

Ushindi huo unaifanya TIMAD FC kuandika historia katika mashindano hayo, huku ukisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika soka la vijana ili kuwajengea mazingira ya kukuza vipaji na kupata fursa ya kushiriki katika ngazi za juu za ushindani.











Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.