MOSHI-KILIMANJARO.
ZAIDI ya watoto 493,680 wenye umri chini ya miaka 10 mkoani Kilimanjaro wanatarajiwa kupata chanjo ya polio katika kampeni maalumu inayolenga kuzuia kuibuka na kusambaa kwa ugonjwa huo unaoweza kusababisha ulemavu wa kudumu.
Hayo yalisemwa juzi na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, wakati akizungumza na viongozi wa Chama na Serikali, viongozi wa dini, viongozi wa mila pamoja na watoa huduma za afya ngazi ya jamii, katika kikao cha maandalizi ya uzinduzi wa kampeni ya utoaji chanjo ya polio kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.
Nzowa alisema Mkoa wa Kilimanjaro umeweka lengo la kuwafikia watoto 493,680 wenye umri chini ya miaka 10, huku akieleza kuwa kampeni hiyo inalenga kuhakikisha watoto wanapata kinga dhidi ya polio na hivyo kuzuia uwezekano wa kuibuka na kusambaa kwa ugonjwa huo.
Alisema kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha watoto wanakingwa dhidi ya polio, hasa kutokana na kuwepo kwa virusi vya ugonjwa huo katika baadhi ya maeneo ya Afrika na uwezekano wa kuingia nchini kupitia mipaka.
“Kampeni hii ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha watoto wanakuwa na kinga dhidi ya polio, kutokana na kuwepo kwa virusi katika baadhi ya maeneo ya Afrika na uwezekano wa kuingia nchini kupitia mipaka,” alisema Nzowa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, aliwahimiza viongozi na wadau kuhakikisha hakuna mtoto hata mmoja mwenye umri chini ya miaka 10 anayeachwa katika kampeni hiyo ya chanjo.
Babu alisema Serikali inalenga kuhakikisha watoto wanakingwa dhidi ya polio na kuwa na afya njema ili waweze kupata fursa ya kusoma, kukua vizuri na kutimiza ndoto zao.
“Tusikubali mtoto yeyote mwenye umri unaolengwa kukosa chanjo. Ni jukumu letu kuhakikisha kila mtoto anafikiwa na kupata kinga dhidi ya ugonjwa huu,” alisema.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Jairy Khanga, aliwataka viongozi na wadau mbalimbali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo hiyo, akisisitiza ushirikiano wa jamii katika kuhakikisha watoto wote wanaolengwa wanapata chanjo.
Alisema chanjo hiyo itatolewa kwa awamu mbili, hatua inayolenga kuhakikisha kila mtoto anayelengwa anapata dozi zote mbili kwa ajili ya kuongeza ulinzi dhidi ya ugonjwa huo.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mercey Mollel, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Ibrahimu Urio, alisema chanjo ni nguzo muhimu katika kuzuia madhara makubwa yanayoweza kusababishwa na polio kwa watoto.
Urio aliwahimiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo zote zinazopendekezwa na wataalamu wa afya, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuwakinga dhidi ya ugonjwa unaoweza kusababisha kupooza na madhara ya kudumu.
“Chanjo ya Polio ina umuhimu mkubwa kwa mtoto kwa sababu inamsaidia kupata kinga dhidi ya ugonjwa unaoweza kusababisha kupooza na madhara ya kudumu, ninawahimiza wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata dozi zote zinazopendekezwa na wataalamu wa afya,” alisema Urio.
Kampeni ya utoaji wa chanjo ya Polio kwa awamu ya kwanza ilizinduliwa Agosti 27, mkoani Kilimanjaro, katika Kituo cha Afya Pasua, ambapo uzinduzi wa Kitaifa ukifanyika mkoani Manyara, Wilaya ya Kiteto.
















