DC MNZAVA; AWATAKA WADHAMINI KUENDELEA KUUNGA MKONO ZUBERI CUP

MOSHI-KILIMANJARO.



MKUU wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amewashukuru wadhamini wa mashindano ya Zuberi Cup kwa namna walivyoendelea kuunga mkono maendeleo ya michezo na kutoa fursa kwa vijana kuonyesha vipaji vyao.

Mnzava ameyasema hayo wakati wa kilele cha mashindano ya Zuberi Cup msimu wa sita, yaliyofikia tamati kwa Kili Wonders FC kutwaa ubingwa baada ya kuifunga Kilimanjaro Plantation FC mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliofanyika Uwanja wa Railway Njoro, Moshi.

Amesema mchango wa wadhamini umeifanya Zuberi Cup kuwa jukwaa muhimu kwa vijana, huku akitaja wadhamini mbalimbali walioshiriki katika mashindano hayo, akiwemo Vodacom, Azania Bank, Razack Builders na GoodLife Gin.

“Tunawashukuru sana wadhamini wengi kupitia mashindano haya ya Zuberi Cup. Tumeona Vodacom, Azania Bank, Razack Builders, GoodLife Gin pamoja na wengine wengi. Niwaombe kuendelea kudhamini mashindano haya,” amesema Mnzava.

Aidha, amezipongeza timu zote zilizoshiriki mashindano hayo kwa kujituma na kutoa ushindani mkubwa, hali ambayo amesema imewapa mashabiki na wapenzi wa soka burudani na fursa ya kushuhudia vipaji mbalimbali vya vijana.

Mnzava pia amepongeza Chama cha Soka Mkoa wa Kilimanjaro (KRFA) pamoja na Chama cha Soka Wilaya ya Moshi kwa usimamizi, uratibu na uendeshaji mzuri wa mashindano hayo hadi kufikia tamati.

“Ninaviomba vyama hivi viendelee kuwa walezi wazuri wa vilabu vya mpira wa miguu,” amesema Mnzava.

Katika hatua nyingine, Mnzava amempongeza mdhamini wa mashindano hayo, Zuberi Abdallah Kidumo, ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Moshi, kwa kujitolea kwake katika kuendeleza mchezo wa soka na kuanzisha mashindano hayo ambayo yamekuwa yakitoa fursa kwa vijana.


Amesema mashindano hayo yamekuwa pia chombo cha kuwaunganisha wananchi na vijana, huku akieleza kuwa idadi kubwa ya mashabiki waliojitokeza viwanjani wakati wa mashindano hayo ni ishara ya namna Zuberi Cup ilivyokubalika katika jamii.

“Tumeshuudia namna wananchi walivyokuwa wakijitokeza kwa wingi na kuja kuona mashindano haya, ambayo yametoa fursa ya kuwakutanisha vijana na wananchi kwa amani na upendo katika kipindi chote cha mashindano,” amesema.

Amesema Zuberi Cup imekuwa daraja muhimu la kutambua na kukuza vipaji vya wachezaji, akibainisha kuwa baadhi ya wachezaji wanaoshiriki Ligi Kuu ya NBC wamepitia katika mashindano hayo.

“Mashindano haya yamekuwa daraja kubwa la kuona vipaji vya wachezaji na namna mashindano haya yalivyofanikiwa kutoa wachezaji wakubwa ambao wanachezea vilabu mbalimbali vya NBC Premier League. Hata leo tunapofunga mashindano haya, wako wachezaji wenye uwezo mkubwa ambao wanaweza kucheza Championship na Ligi Kuu,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Kilimanjaro, Isaac Gaga, amesema wameendelea kushuhudia ukuaji wa mchezo wa soka nchini, hususan mkoani Kilimanjaro, kutokana na kuongezeka kwa mashindano na fursa kwa vijana.

Gaga amesema uwepo wa mashindano mbalimbali mkoani humo, yakiwemo Samia-Hai, Koola Vunjo Cup na Zuberi Cup, ni sehemu ya mazingira yanayowawezesha vijana kushiriki michezo na kukuza vipaji vyao.

“Yako mashindano ambayo yamekuwa yakiendelea, ya Samia-Hai, Mashindano ya Vunjo Koola Cup na hapa Moshi ya Zuberi Cup. Yote hii ni kutokana na amani na utulivu uliopo katika Taifa letu,” amesema Gaga.

Aidha, amesema mafanikio ya soka mkoani Kilimanjaro yanaonekana pia kupitia timu zilizofanikiwa kupata nafasi ya kushiriki ligi za juu, akitaja timu ya Polisi Tanzania pamoja na timu ya wanawake ambazo zinatoka mkoani humo.

Amesema pia kuna timu ya Ensduimet kutoka Wilaya ya Siha inayoshiriki mashindano ya FEST, huku Kili Wonders ikiwa miongoni mwa timu zinazowekeza katika vijana wenye umri mdogo.

Gaga amesema wachezaji 15 wenye umri chini ya miaka 20 kutoka Kili Wonders wamechukuliwa na Polisi Tanzania kwa ajili ya kuendelea kunolewa na kuendelezwa zaidi, akisema hatua hiyo ni miongoni mwa mafanikio makubwa yanayoonyesha matokeo ya uwekezaji katika soka mkoani Kilimanjaro.

Amesema hatua hiyo inapaswa kuwa chachu kwa wadau wengine kuendelea kuwekeza katika mashindano ya vijana ili kutoa kizazi kipya cha wachezaji watakaoliwakilisha taifa katika ngazi mbalimbali.

Mashindano ya Zuberi Cup msimu wa sita yamehitimishwa kwa Kili Wonders FC kutwaa ubingwa baada ya kuifunga Kilimanjaro Plantation FC mabao 2-0, huku mashindano hayo yakitajwa kuwa miongoni mwa majukwaa muhimu ya kukuza vipaji vya soka mkoani Kilimanjaro.












Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.