ZUBERI CUP YATANGAZA ZAWADI ZA MABINGWA, WASHINDI WA PILI NA TATU



MOSHI-KILIMANJARO.

KAMATI ya Mashindano ya Zuberi Cup imetangaza zawadi ambazo zitakabidhiwa kwa timu zitakazomaliza katika nafasi ya kwanza, ya pili na ya tatu, huku bingwa wa mashindano hayo akitarajiwa kujinyakulia kitita cha Sh milioni 2.5 pamoja na zawadi nyingine.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo, Japhet Mpande, amesema hayo wakati wa kikao na waandishi wa habari kilichofanyika ofisini kwake, akieleza kuwa mshindi wa kwanza atakabidhiwa kikombe, medali, jezi seti moja, mpira mmoja pamoja na Sh milioni 2.5 taslimu.

Mpande amesema mshindi wa pili atapata Sh milioni 2, medali, jezi seti moja pamoja na mpira, wakati timu itakayomaliza katika nafasi ya tatu itajinyakulia Sh milioni moja.

Aidha, amesema tuzo za mchezaji bora, golikipa bora, kocha bora pamoja na mfungaji bora zitatolewa kwa ushirikiano na Benki ya Azania, ambayo itahusika na kukabidhi zawadi kwa washindi wa tuzo hizo.

Katika hatua nyingine, Mpande ametangaza kuwa mchezo wa fainali ya Zuberi Cup utachezwa Agosti 23, 2026, katika Uwanja wa Railway Njoro, Moshi, huku akiwashukuru mashabiki na watazamaji waliojitokeza kwa wingi kuanzia hatua za mwanzo za mashindano hadi hatua ya sasa.

Amesema kamati pia inawashukuru wadhamini wa mashindano hayo kwa mchango wao, pamoja na waandishi wa habari ambao wamekuwa wakifika viwanjani na kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya mashindano hayo kwa kipindi chote.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.