KILI PLANTATION FC YATINGA FAINALI ZUBERI CUP, BAADA YA KUICHAPA HAI UNITED

MOSHI-KILIMANJARO.

TIMU ya Kili Plantation FC imefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya mashindano ya Zuberi Cup baada ya kuichapa Hai United bao 1-0 katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Railway Njoro, Moshi.

Mchezo huo ulikuwa wa ushindani mkubwa, huku timu zote zikionyesha nia ya kutafuta ushindi na kujihakikishia nafasi ya kucheza fainali, hata hivyo, Kili Plantation FC ndiyo iliyofanikiwa kupata bao pekee la mchezo huo.

Bao hilo lilifungwa dakika ya 27 ya kipindi cha kwanza na David Sanga, aliyefunga baada ya mpira wa kona kuingia wavuni na kuiwezesha Kili Plantation FC kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili, Hai United iliongeza mashambulizi ikitafuta bao la kusawazisha, huku Kili Plantation FC ikijikita zaidi katika kulinda uongozi wake na kutumia nafasi za kushambulia kupitia mashambulizi ya kushtukiza.

Juhudi za Hai United hazikuzaa matunda hadi mwamuzi alipuliza filimbi ya mwisho, Kili Plantation FC ikitoka uwanjani na ushindi wa bao 1-0 na kutinga rasmi hatua ya fainali.

Katika fainali itakayochezwa Agosti 23, 2026, Kili Plantation FC itakutana na Kilimanjaro Wonders FC, katika mchezo unaotarajiwa kuwa wa ushindani mkubwa kutokana na ubora wa timu zote mbili na hatua waliyofikia katika mashindano hayo.

Kabla ya fainali hiyo, mchezo wa kusaka mshindi wa nafasi ya tatu utachezwa Agosti 22, 2026, ambapo La Familia FC itakutana na Hai United kuanzia saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Railway Njoro.



















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.