WADHAMINI WAPONGEZA ZUBERI CUP KWA KUUNGANISHA VIJANA, KUIBUA VIPAJI

MOSHI-KILIMANJARO.

WADHAMINI wa mashindano ya mpira wa miguu ya Zuberi Cup wamepongeza namna mashindano hayo yalivyogeuka kuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha vijana, kukuza vipaji na kutoa fursa kwa wachezaji wenye uwezo kuonyesha vipaji vyao katika mchezo wa mpira wa miguu.

Wakizungumza baada ya kumalizika kwa mashindano hayo yaliyofikia kilele kwa timu za Kili Wonders FC na Kilimanjaro Plantation FC kukutana katika mchezo wa fainali uliofanyika kwenye Uwanja wa Railway Njoro, wadhamini hao wamesema Zuberi Cup imekuwa na mchango mkubwa katika kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia vipaji vya vijana.

Meneja Masoko kutoka kampuni ya Mark Beverages Tanzania, watengenezaji wa kinywaji cha GoodLife Gin, Erick George, amesema kampuni hiyo imekuwa sehemu ya familia ya Zuberi Cup na imefurahishwa na namna mashindano hayo yalivyowaunganisha vijana kutoka maeneo mbalimbali.

“Tumekuwa sehemu ya familia ya Zuberi Cup, mashindano ambayo yameunganisha vijana kwa pamoja,” amesema George.

Amesema ushiriki wao katika mashindano hayo umetokana na kutambua umuhimu wa vijana katika jamii, akieleza kuwa kampuni hiyo imeamua kuwa sehemu ya juhudi zinazolenga kuwawezesha vijana kutumia vipaji vyao katika michezo.

“Lengo letu ni kuwa karibu na vijana, na umoja ambao umeonekana katika mashindano haya ni jambo kubwa.

Kwa mara ya kwanza tumeweza kushiriki kuwa sehemu ya wadhamini katika msimu huu, na tunaahidi kuendelea kuwa sehemu ya wadhamini wa mashindano haya hususan katika msimu ujao mambo yatakuwa makubwa zaidi,” amesema.

Akizungumzia bidhaa yao, George amesema GoodLife Gin ni miongoni mwa vinywaji vinavyotengenezwa kwa kuzingatia viwango vya ubora, huku akitaja mwonekano na ladha yake kuwa ni miongoni mwa mambo yanayowavutia watumiaji.

Amesema kampuni hiyo inaendelea kupanua upatikanaji wa bidhaa zake katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Arusha, Manyara na Kilimanjaro.

Naye Meneja wa Azania Bank, Tawi la Moshi, Yusuph Lenga, amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na mashindano ya Zuberi Cup kutokana na nafasi yake katika kuwaunganisha vijana na jamii kwa ujumla.

Lenga amesema michezo ni moja ya maeneo muhimu yanayoweza kuwasaidia vijana kutumia muda wao vizuri, kujenga vipaji na kupata fursa za kuendeleza ndoto zao, hivyo ni muhimu wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono mashindano ya aina hiyo.

Amesema Azania Bank inatambua umuhimu wa kuwa sehemu ya shughuli zinazogusa jamii na kwamba ushiriki wao katika Zuberi Cup ni sehemu ya kuunga mkono maendeleo ya vijana kupitia michezo.

Kwa upande wake, Mhandisi Zuberi Kidumo, ambaye ni mdhamini wa mashindano hayo, amewapongeza wadhamini wote waliojitokeza kuunga mkono mashindano hayo, akisema mchango wao umewezesha Zuberi Cup kufikia mafanikio makubwa.

Kidumo amesema ushirikiano wa wadhamini mbalimbali umeonyesha kuwa mashindano hayo si tukio la michezo pekee, bali ni sehemu ya kujenga mazingira bora kwa vijana kuonyesha vipaji vyao, kujifunza na kujenga mahusiano kupitia michezo.

Amesema uwepo wa wadhamini umeongeza nguvu katika mashindano hayo na kuwapa hamasa waandaaji kuendelea kuyaboresha katika misimu ijayo.

“Binafsi nawashukuru sana wadhamini Azania Bank, Vodacom, Razack Builders na GoodLife Gin kwa namna walivyonishika mkono na kufanikisha mashindano, ahadi yangu ni kwamba msimu unaokuja tutakwenda kufanya vizuri zaidi tofauti na msimu uliopita,” amesema Kidumo.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amewashukuru wadhamini waliojitokeza kuunga mkono mashindano ya Zuberi Cup, akisema ushiriki wao umeonyesha namna sekta binafsi inavyoshirikiana na Serikali katika kuendeleza na kukuza michezo nchini.

Amesema mchango wa wadhamini umeiwezesha Zuberi Cup kukua na kuwa jukwaa muhimu la vijana kushiriki michezo, huku akiwataka kuendelea kushirikiana na waandaaji wa mashindano hayo katika misimu ijayo.

“Tunawashukuru sana wadhamini, kupitia mashindano haya ya Zuberi Cup, tumewaona Vodacom, Azania Bank, Razack Builders, GoodLife Gin pamoja na wengine wengi. Niwaombe kuendelea kudhamini mashindano haya,” amesema Mnzava.

Mashindano ya Zuberi Cup yameendelea kuwa miongoni mwa mashindano yanayotoa jukwaa kwa timu mbalimbali za vijana kushindana, huku yakivuta idadi kubwa ya mashabiki na wadau wa soka katika maeneo mbalimbali ya Moshi na Kilimanjaro.














Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.